AKILI ZA KIJIWENI: Mashabiki wasikashfiwe Taifa Stars

TAIFA Stars imetupa heshima sana baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea katika mechi ya raundi ya pili ya hatua ya makundi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

Kabla ya hapo Stars ilitoka suluhu na Ethiopia katika mechi ya kwanza iliyochezwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya ushindi dhidi ya Guinea kumeibuka kundi la watu ambao wanawazodoa mashabiki na wadau wa soka ambao hawakufurahishwa na matokeo ya mechi ya kwanza dhidi ya Ethiopia ambayo ilimalizika kwa matokeo ya sare tasa.

Yote ni kwa sababu mashabiki na wadau hao walishangazwa na namna kikosi cha mchezo wa kwanza kilivyopangwa ambacho benchi la ufundi la kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ liliwaanzisha wachezaji wanane wenye asili ya ulinzi kwenye uwanja wa nyumbani.

Pia kikosi kilivyocheza waliamini haikutakiwa kuwa hivyo kwa hiyo imani yao ni kwamba kuna namna benchi la ufundi halikuwatendea haki katika mechi hiyo ambayo kama tungeshinda leo tungekuwa katika nafasi nzuri katika Kundi H.

Naamini mashabiki na wadau hawatakiwi kusutwa kisa tumepata ushindi dhidi ya Guinea maana ambacho walikilalamikia hakikuwa kwa mlengo wa chuki bali ni kutaka kuona timu inafanya vizuri.

Waliamini mchezaji kama Mudathir Yahya anahitajika kupata muda mwingi wa kucheza na hakutakiwa kuchelewa kuingia na hilo limezaa matunda dhidi ya Guinea ambapo amecheza kwa muda mwingi na akaifungia timu bao la ushindi.

Watu waondoe dhana kuwa mashabiki na wadau wanaokosoa sio maadui na wale wanaosifia sio wapambe.

Wote tamaa yao ni kuona Stars inashinda hivyo isipopata ushindi sio wote wanaweza kuwa na ustahamilivu wa kupokea matokeo ya kufungwa.

Hakuna shabiki anayechukia timu inaposhinda na hakuna shabiki anayefurahi timu isiposhinda.