Aliyehukumiwa miaka 20 jela kwa kusafirisha wahamiaji haramu aachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya, imemuachia huru Nyalobi Kibona, aliyekuwa amehukumiwa kulipa faini ya Sh20 milioni au kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha wahamiaji haramu 43.

Nyaboli alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, katika kesi ya jinai namba 130 ya mwaka 2022 ambapo alidaiwa kusafirisha wahamiaji haramu hao kinyume na kifungu cha 46 (1) (c) (g) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za rufaa, ilidaiwa Mei 24, 2022 katika eneo la Mkora, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Nyaboli alikutwa akiwasafirisha wahamiaji haramu 43 raia wa Ethiopia kwa kutumia gari lililokuwa na namba za usajili T306 ANX, Mitsubishi Fuso.

Baada ya kutokuridhika na hukumu hiyo, Nyaboli alikata rufaa hiyo ya jinai namba 17085 ya mwaka 2024 ambapo alikuwa na sababu tano za rufaa.

Jaji Aisha Sinda, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo, alitoa uamuzi huo jana Septemba 11, 2024 ambapo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, alieleza kuwa Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka na ulikuwa umejaa mashaka.

Nyaboli ambaye katika rufaa hiyo hakuwa na uwakilishi wa wakili ambapo aliwasilisha sababu zake za rufaa ambazo ni Mahakama ya chini ilikosea kisheria ilipomtia hatiani na kumhukumu bila kuzingatia hakukamatwa eneo la tukio akiwasafirisha wahamiaji haramu hao.

Nyingine ni Mahakama ilikosea kisheria ilipomtia hatiani na kumhukumu bila kuzingatia kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwaita wahamiaji haramu hao ili kuthibitisha kuwa mrufani ndiye alikuwa akiwasafirisha.

Hoja nyingine ilikuwa kwamba Mahakama ya awali ilikosea kisheria ilipomtia hatiani na kumhukumu mrufani bila kuzingatia kwamba shahidi wanne kama mmiliki wa gari T309 ANX alishindwa kutoa mkataba wa maandishi kuthibitisha kwamba alikabidhi gari hilo kwake.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa Serikali, Rajabu Msemo ambaye alidai kuwa kupitia mwenendo wa shauri hilo, ushahidi unaonyesha mrufani huyo na mwingine katika siku ya tukio walihusika kusafirisha wahamiaji haramu baada ya kuendesha gari umbali mrefu na wahamiaji hao kuanza kulalamika hakuna hewa.

Alidai kuwa Nyaboli na mwenzake waliondoka na kutelekeza gari hilo ambapo wahamiaji hao walipotolewa kwenye gari hilo na kuulizwa alipo dereva walidai ametoweka na kuwa suala hilo halikupingwa na Nyaboli wakati wa kuhojiwa.

Kuhusu wahamiaji hao haramu kutokuitwa mahakamani kutoa ushahidi, wakili huyo alidai kuwa walipeleka mashahidi wanne ambao waliwezesha mrufani huyo kutiwa hatiani na kuwa hakuna idadi maalumu ya mashahidi ili kuthibitisha kosa.

Kuhusu hoja ya mmiliki wa gari hilo, Bulemo Mafuru (shahidi wa nne), ambaye alidai  kuwa na uhusiano na mrufani huyo na kuwa alimpa gari hilo kwa sababu Nyaboli hakuwa na kazi, na kuwa suala la makubaliano yaliyoandikwa kutokutolewa mahakamani hayana umuhimu na kuomba mahakama kutupilia mbali rufaa hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji Sinda alianza kwa kueleza kuwa masuala muhimu yatakayojadiliwa ni nani aliyekuwa anamiliki gari hilo wakati tukio hilo linatokea na katika kuchambua hilo atazingatia ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu.

Amesema katika kesi hiyo ni jambo lisilopingika kuwa gari hilo lilikuwa linamilikiwa na shahidi wa nne na hilo linathibitishwa na kielelezo cha pili, kilichoonyesha gari limesajiliwa kwa jina la shahidi huyo.

Kuhusu wapi Nyaboli alikuwa akisimamia gari hilo siku ta tukio, Jaji Sinda amesema shahidi wa kwanza alieleza namna walivyokamata wahamiaji haramu hao ila hakutaja waliotenda kosa la kusafirisha wahamiaji hao.

Jaji huyo alieleza kuwa shahidi wa pili katika kesi hiyo aliyedai kuchukua maelezo ya onyo ya mrufani huyo, ambayo yalikataliwa katika mahakama hiyo ya chini kwa sababu mrufani alikana kuandika maelezo hayo.

“Kwa hali hiyo, hakuna shahidi hata mmoja kati ya waliotajwa hapo juu ambaye ametoa ushahidi unaomhusisha moja kwa moja mrufani na kosa hilo, hakuna shahidi hata mmoja kati ya waliotajwa ambaye alitoa ushahidi moja kwa moja unaomhusisha na kosa,” amesema.

Jaji Sinda amesema mashahidi watatu walikuwa muhimu ili kuimarisha kesi ya mashtaka ambao ni mke wa shahidi wa nne (aliyedaiwa kuwa ndugu wa mrufani), dereva wa shahidi hiyo wa nne na wakwe wanaodaiwa kumpokea mrufani huyo katika nyumba yao.

“Mashahidi hawa wangethibitisha uwezekano wa shahidi wa nne kukabidhi gari kwa mrufani, matokeo yake kushindwa kuwaita bila sababu za kutosha inakuwa vigumu sana kuthibitisha gari lilikuwa chini ya usimamizi wa mrufani,” amesema Jaji.

“Katika ukurasa wa 63 wa mwenendo katika aya ya pili, shahidi wa nne alisema kuwa alipewa RB kwa ajili ya kumtafuta mrufani, baada ya mrufani kutoweka na gari bila ridhaa yake ila RB hiyo haikutolewa kama kielelezo mahakamani,” amesema.

Jaji Sinda amesema RB iliyotajwa ilikuwa ushahidi muhimu wa kuthibitisha kwamba Nyaboli alitoweka na gari la Amani na walikuwa wakimtafuta.

Jaji Sinda amesema ushahidi wa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya Nyaboli kwani ulikuwa umejaa mashaka hivyo anakubali rufuaa hiyo na kufuta hukumu na kuamuru Nyaboli aachiwe huru.