Kipenye, Mkomola wapagawisha Songea Utd

SONGEA United imeendelea kujifua kujiweka fiti, huku baadhi ya mastaa wakitoa matumaini kwa mashabiki kuhakikisha Mkoa wa Ruvuma unarejesha heshima kwa kupata timu ya Ligi Kuu.

Timu hiyo ambayo ilifahamika kama FGA Talents, kwa sasa imeweka maskani mjini Songea na inatarajiwa kushiriki Ligi ya Championship msimu ujao itakayoanza mwishoni mwa mwezi huu kusaka kutinga Ligi Kuu ijayo.

Mkoa wa Ruvuma ulikuwa ukijivunia Majimaji Songea ‘Wanalizombe’ waliokuwa wakizipeleka Simba na Yanga, lakini kwa zaidi ya misimu mitano wadau na mashabiki hawajaonja tena ladha ya Ligi Kuu baada ya timu hiyo kushuka daraja na kupoteana.

Hata hivyo, kwa sasa wadau na mashabiki wengi wameelekeza macho na masikio kwa Songea United wakiamini inaweza kuwarejeshea furaha ya Ligi Kuu waliyoikosa.

Hadi sasa timu hiyo inaendelea kujifua Dar es Salaam ilikoweka kambi yake, huku ikijivunia usajili wa baadhi ya mastaa waliowahi kutamba ndani na nje ya nchi wakiwamo Cyprian Kipenye na Yohana Mkomola.

Meneja wa timu hiyo, Shaaban Ibrahim alisema wamekuwa na maandalizi mazuri na muda wa kutosha kuandaa vijana kwa ajili ya msimu ujao na matarajio yao ni kufanya vizuri na kupanda Ligi Kuu.

Alisema kwa sasa timu ipo chini ya kocha msaidizi, Ivo Mapunda wakati uongozi ukiendelea na mchakato wa kumtafuta kocha mkuu, kufuatia dili la Mohamed Badru kugonga mwamba dakika za mwisho.

“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi, tumekuwa na mechi kadhaa za kirafiki na tumeshinda zote ikiwamo Green Warriors na Copco, kiujumla matumaini ni makubwa kwa timu yetu,” alisema meneja huyo.