Mwana FA: Watanzania msiisuse Taifa Stars

NAIBU Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma “Mwana FA” amewaomba Watanzania kutoisusa timu yao ya Taifa Stars pindi inapokuwa inapata changamoto ya matokeo.

Kauli ya kiongozi huyo imekuja kutokana na Watanzania kuonekana kukata tamaa baada ya Stars kutoka suluhu dhidi ya Ethiopia nyumbani katika mchezo wa kwanza wa kufuzu Afcon kabla ya kushinda ugenini dhidi ya Guinea.

Naibu Waziri huyo amewaomba Watanzania wasiwe katika hali hiyo, kwani hakuna wa kumwachia majukumu ya kuisapoti Stars zaidi ya Watanzania wenyewe.

Ameyasema hayo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam akiambatana na timu ya Stars, iliyotoka nchini Ivory Coast kucheza dhidi Guinea.

“Mtoto akiunyea mkono huwezi kuukata, utausafisha maisha mengine yanaendelea, hakuna anayefurahishwa na kukosa matokeo ya ushindi, hivyo niwaombe, tukifungwa tufungwe wote, tukishinda tushinde wote na tufurahi wote,” alisema.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alimkabidhi Mwana FA shilingi milioni 10 aliyoagizwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili kuwapa wachezaji Stars ikiwa ni ahadi yake ambapo Nahodha Himid Mao alizipokea fedha hizo kwa niaba ya wachezaji wenzake.

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, amesema: “Ushindi huu ni wa Watanzania wote, tunashukuru kwa kutuunga mkono, tutaendelea kufanya vizuri zaidi katika michezo iliyopo mbele yetu.”

Kiungo mshambuliaji wa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alisema: “Tunawashukuru Watanzania kutuunga mkono, wasichoke, bado kazi ipo ngumu mbele yetu, waendelee kutuunga mkono.”

Kiungo mkabaji na nahodha wa Stars, Himid Mao anayecheza soka la kulipwa Misri, alisema: “Watanzania timu ya Stars ni ya kwenu, katika hali zote tunaomba kutuunga mkono, tunashukuru mheshimiwa Rais Samia Suluhu kutuunga mkono.”

Stars inacheza mechi za kuwania kufuzu michuano ya Afcon itakayopigwa nchini Morocco mwaka 2025.

Baada ya Stars kushinda dhidi ya Guinea mabao 2-1, ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi H, ikiwa na pointi nne, inayoongoza ni DR Congo iliyo na pointi sita. Ethiopia ina moja na Guinea haina kitu.