Sare yaipeleka KVZ kileleni ZPL

MAAFANDE wa KVZ juzi jioni walilazimishwa suluhu na wageni wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Tekeleza FC ya kisiwani hapa na kukwea hadi kileleni mwa msimamo ikiwaengua watetezi, JKU.

Tekeleza iliyopanda daraja msimu huu sambamba na Junguni pia ya Pemba na Muembe Makundi na Inter Zanzibar za visiwani Unguja, pointi moja iliyovuna katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, umeifanya ichomoke mkiani na kuchupa hadi nafasi ya 10, huku KVZ ikipaa kileleni ikifikisha pointi nne baada ya kila moja kucheza mechi mbili (hii ni kabla ya mechi tatu za leo).

Tekeleza ilianza msimu mpya kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa maafande wengine wa Kipanga, huku KVZ ikishinda bao 1-0 mbele ya Mwenge, na katika mechi ya juzi kila moja ilionyesha soka tamu ikitaka kuondoka na pointi tatu, lakini milango ya timu zote ilikuwa migumu hadi dakika 90.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya pambano hilo, mahodha wa Tekeleza, Suleiman Ali Hamad alisema bado kikosi chao ni kigeni kutoka na ukweli wanashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, hivyo taratibu wanajifunza na kuizoea na wanashukuru kuvuna pointi moja mbele ya maafande hao wa KVZ.

“Tushashuru kwa kupata alama hii moja, tulikuwa tunahitaji sana ushindi katika mchezo na KVZ maana mchezo wetu wa kwanza tulipoteza mbele ya Kipanga, ukweli bado tutajipanga zaidi,” alisema Suleiman, huku kocha mkuu wa KVZ, Ali Mohamed Amer akisema hakutarajia kupata matokeo hayo akidai kwa usajili mzuri aliofanya kwenye kikosi chake bado haujaendana na matarajio ya kikosi chao.

Alisema kwa vile ni mapema, tayari wameshaona dosari na wanakwenda kuzifanyia kazi, kwani pointi moja ugenini si haba kuliko ingepoteza.

Ligi hiyo ya Zanzibar ilianza wikiendi iliyopita na sasa ipo raundi ya pili, huku wageni wa michuano hiyo, Muembe Makumbi ndio pekee walioonyesha uhai hadi sasa kwa kushinda dhidi ya New City, wakati Junguni na Inter Zanzibar zikianza kwa vipigo kila moja ikifungwa mabao 3-1 kama ilivyokuwa kwa Tekeleza kabla ya juzi kuzinduka kwa suluhu nyumbani na leo itaendelea tena kwenye viwanja viwili.