Arumeru. Ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotokana na utumikishwaji watoto hasa kwenye masoko na stendi, shirika lisilokuwa la kiserikali la Save the Children limetoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wafanyabiashara katika Soko la Tengeru lililoko wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.
Elimu hiyo imetolewa leo ikiwa ni mwendelezo wa wiki ya Azaki inayoendelea mkoani Arusha na kushirikisha wadau zaidi ya 500.
Akizungumza na wafanyabiashara hao katika soko hilo,Meneja wa Miradi kutoka Mkoa wa Dodoma wa Shirika la Save the Children,Mariam Mwita,amesema wamechagua kutoa elimu kwa kundi hilo kwani wengi wao wamekuwa wakitumikishwa katika masoko na vituo vya mabasi.
Amesema mbali na elimu hiyo wamekuwa wakihamasisha elimu ya lishe kwa kaya lengo likiwa ni kuboresha afya na lishe kwa watoto.
“Elimu hii imegusa maeneo ya utumikishwaji wa watoto masokoni na kuhusu masuala ya lishe,usafi wa mazingira na tumekuwa tukiitoa kwa makundi mbalimbali ili kuwakumbusha wajibu wa malezi na kuepukana na kuwatumikisha watoto,”amesema
“Uchumi wa wananchi ukiimarika watoto wataondokana na ukatili wa kijinsia kwa kuwa watapata mahitaji yao ya msingi ikiwamo chakula, mavazi na malazi,”amesema
Ofisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Meru,Martha Mzava, amesema katika hatua ya kukabiliana na matukio hayo,wanatoa elimu ngazi za kata, kwenye mikutano ya vijiji,pia wameunda Kamati za Kupambana na Kupinga Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwa).
Amesema kamati hizo zimelenga kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.