Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bariadi afariki dunia

Simiyu. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Juliana Mahongo amefariki dunia.

Katibu wa CCM wilaya ya Bariadi, Ibrahim Kijanga akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kifo cha mwanasiasa huyo ambacho amedai kimetokea leo Jumapili Septemba 15, 2024, Saa 1:00 asubuhi akiwa nyumbani kwake mtaa wa Somanda mjini Bariadi.

“Ni kweli Mwenyekiti amefariki dunia akiwa nyumbani kwake maeneo ya Somanda na kwa sasa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kusubiri taratibu za mazishi,” amesema Kijanga.

“Kuhusu taratibu za mazishi tunasubiri kutoka kwa familia ambao wao watakijulisha chama na wananchi tutawajulisha kuwa ni wapi na lini mazishi yatafanyika,” amesema.

Mwenyekiti huyo hadi amekutwa na mauti amekuwa akihudumu katika nafasi hiyo kwa vipindi vinne mfululizo.

Amesema kuwa taarifa ya chanzo cha kifo hicho pamoja itatolewa na familia sambamba na mipango ya mazishi inaandaliwa na familia na itakapokamilika CCM wilaya ya Bariadi itajulishwa na kutoa taarifa kwa wananchi.

Katibu huyo amemtaja marehemu Mahongo kama kiongozi ambaye alikuwa mtiifu, mwaminifu na mzalendo kwa chama chake.

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital