Dar es Salaam. Unajihisi salama kiasi gani unapokuwa katika zahanati, kituo cha afya au hospitali unapatiwa huduma za matibabu ya maradhi au jeraha lolote?
Swali hilo linaakisi uhalisia wa wanayoyapitia baadhi ya wagonjwa wanapokuwa katika huduma za matibabu, ama wapone au kusababishiwa matatizo zaidi na hatimaye kupoteza maisha.
Athari za matibabu kwa wagonjwa aghalabu, husababishwa na changamoto ya umakini wa wataalamu wa afya na wakati mwingine usimamizi duni wa huduma ya mgonjwa baada ya matibabu.
Kutokana na uhalisia huo, mwaka 2019, Shirika la Afya Duniani (WHO), lilianzisha Siku ya Usalama wa Wagonjwa inayoadhimishwa Septemba 17 kila mwaka, kama sehemu ya kampeni ya kimataifa ya kuboresha usalama katika sekta ya afya.
Umuhimu wa siku hiyo, unatokana na uhalisia wa madhira yanayowatokea wagonjwa kwa makosa ya matibabu kama inavyobainishwa katika ripoti ya WHO ya mwaka 2020.
Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa, kila mwaka makosa yanayohusiana na huduma za afya husababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 2.6 duniani.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wagonjwa wengi hupata madhara kutokana na huduma zisizo salama au makosa ya kimatibabu.
Ripoti hiyo imekwenda mbali zaidi na kuonyesha, katika kila wagonjwa 1,000 kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati, 134 hupata madhara wanapopokea huduma za afya.
Hata hivyo, utafiti wa mwaka 2021 wa shirika hilo, uliweka wazi, matukio hayo yanayowakumba wagonjwa kwa asilimia 50 yanaweza kuzuilika kwa kutumia mifumo ya usimamizi na mafunzo bora kwa wahudumu wa afya.
Kama unastaajabu takwimu za ulimwengu, yanayotokea Tanzania yatakushangaza.
Takwimu za Wizara ya Afya mwaka 2022, ziliweka wazi kuwa, katika kila wagonjwa 1,000 wanaolazwa hospitalini, 15 hupata madhara yatokanayo na makosa ya kimatibabu.
Hilo linaenda sambamba na takwimu za maambukizi ya hospitalini zinazoeleza asilimia 25 ya wagonjwa wanaopata huduma za upasuaji nchini hupata maambukizi.
Siku hii ilipitishwa mwaka 2019 kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye mkutano wa 72 wa afya duniani mwaka huo kwa maazimio yenye ujumbe usemao: ‘Hatua za Kimataifa kwa Usalama wa Wagonjwa.’
Wadau wakuu kitaifa na kimataifa wamekuwa wakishiriki katika kukuza na kupigia chapuo usalama wa wagonjwa, kupitia tukio hilo muhimu la kila mwaka.
Kabla ya kuanzishwa kwa siku ilitanguliwa na ‘Wiki ya Usalama wa Wagonjwa’ ambayo ilikuwa inaanza Machi 10 hadi 16 kila mwaka. Katika wiki hii, mashirika ya afya na wataalamu huwa wanaweka mkazo mkubwa katika kuboresha usalama wa huduma za afya kwa kila mtu.
Hii ni wakati wa kusherehekea maendeleo yaliyopatikana katika usalama wa wagonjwa na kutambua juhudi zinazohitajika kuendeleza usalama wa huduma za afya.
Maadhimisho haya yanasisitiza kuzuia madhara katika mazingira ya huduma za afya, jambo linalobaki kuwa tatizo kubwa la afya ya umma.
Kwa kuwa takwimu zinazoonyesha makosa ya matibabu yanayoweza kuepukwa yanaweza kusababisha vifo vya mamia ya maelfu kila mwaka, wiki hii ina jukumu muhimu katika kuendeleza mazoea salama ya huduma za afya.
Kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wagonjwa, watoa huduma za afya, na umma, lengo likiwa kuchochea utamaduni wa usalama ambao ni muhimu kwa utoaji wa huduma za afya wenye ufanisi.
Siku hii kwa namna itakavyoadhimishwa inatoa fursa ya elimu na kuhamasisha jamii. Inasisitiza uwazi, uongozi na sera zinazohakikisha ustawi wa wagonjwa.
Kupitia shughuli na rasilimali zinazoshirikiwa katika wiki hii, kampeni inahimiza kila mmoja anayehusika na wagonjwa kuanzia ngazi ya familia na wataalamu wa afya kuchangia katika mazungumzo na hatua zinazoboresha usalama katika viwango vyote vya huduma.