Rais Samia ang’aka, azijibu balozi za Umoja wa Ulaya

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amejibu matamko ya balozi zinazowakilisha mataifa mbalimbali nchini, yaliyotaka uchunguzi wa haraka wa matukio ya utekaji na mauaji ya watu, akisema Tanzania ni nchi huru haipaswi kuelekezwa cha kufanya kwenye mambo yake.

Katika majibu yake hayo, amewashutumu mabalozi hao akisema walichokitamka haamini kama ni maelekezo ya wakuu wa nchi zao, huku akiahidi kuwachongea kwa marais wa mataifa husika kwa kuiingilia Tanzania.

Chimbuko la majibu ya mkuu huyo wa nchi ni tamko la pamoja la balozi za mataifa 15 yanayowakilisha Umoja wa Ulaya (EU) nchini, yakilaani na kutaka uchunguzi wa haraka na huru wa matukio ya mauaji.

Balozi zilizotoa tamko hilo la pamoja ni Ubelgiji, Uingereza, Canada, Denmark, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Hispania, Sweeden na Uswisi.

Pia, Marekani ilitoa tamko la peke yake juu ya matukio hayo.

Katika tamko hilo, balozi hizo zilisema: “Tunakaribisha wito wa Rais wa kuanzisha uchunguzi wa haraka ili kubaini wahalifu waliohusika na kuhakikisha kuna uwajibikaji.”

Kadhalika wametaka ulinzi wa upinzani, ili kuakisi falsafa ya 4R ya Rais Samia na kusisitiza:“Tunatambua kwa wasiwasi mkubwa kwamba matukio haya ya hivi karibuni yanatishia misingi ya kidemokrasia na haki za wananchi wa Tanzania.”

Hata hivyo, mabalozi hao walitoa tamko hilo, muda mchache baada ya taarifa ya kifo cha kada wa Chadema, Ali Kibao aliyechukuliwa akiwa katika usafiri wa umma Septemba 6, mwaka huu na siku moja baadaye amekutwa ameuawa.

Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 17, 202, Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Maofisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi na miaka 60 ya Jeshi la Polisi.

“Hatupo hapa kuelekezwa nini cha kufanya ndani ya nchi yetu, tuna Katiba sheria, miongozo, mila na desturi zetu zinazotuongoza nini cha kufanya kwenye nchi zetu,” amesema.

Rais Samia amesema ameapa kuilinda na kuitetea nchi na kwamba atafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa Watanzania kwa kuwa ni jukumu lake.

Katika wajibu huo, amesema hahitaji kuelekezwa na mtu yeyote cha kufanya kwa sababu Katiba ya Tanzania ina maelekezo ya jinsi ya kuendesha Serikali.

“Wengine wanapotaka kuonyesha huruma yao basi tunawasihi wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya mahusiano kidiplomasia ya kimataifa kama ilivyoelezwa kwenye Vienna Convention on Diplomatic Relation la 1961.

“Lile tamko lililotoka na kuambiwa tufanye moja mbili tatu, sisi tunajua cha kufanya kama Tanzania kama nchi yetu. Na ni imani yangu kwamba tamko lile lililotolewa si maelekezo ya wakuu wa nchi huko walikotoka,” amesema.

Kwa sababu ana namna ya kujua, mkuu huyo wa nchi amesema atawasiliana na wakuu wenzake wa nchi za balozi hizo kujua iwapo tamko hilo ni maelekezo yao na kama sivyo atawasilisha malalamiko yake.

Katika maelekezo yake hayo, amesema mauaji yanatokea katika kila nchi, lakini Tanzania haikuwahi kuwatuma mabalozi wake wakaelekeze nchi hizo cha kufanya.