Uchovu wapunguza mabao Azam | Mwanaspoti

KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema kuwa timu yake ilipata ushindi mgumu dhidi ya Coastal Union ya Tanga kutokana na uchovu uliowakumba wachezaji baada ya mechi mbili mfululizo ndani ya siku chache.

Taoussi alieleza kuwa timu yake haikuwa na nafasi nyingi za kufunga dhidi ya Coastal Union jambo lililochangiwa na kukosa muda mwingi wa kupumzika tangu ilipotoka kucheza mchezo wa mwisho.

Kocha huyo raia wa Morocco alibainisha hayo baada ya juzi Jumapili kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Kabla ya hapo, Alhamisi iliyopita walishinda kwa maba 4-0 dhidi ya KMC.

“Hatukuwa na nafasi nyingi za kufunga, tulipata bao moja tu, lakini tumecheza baada ya mapumziko ya saa 48 tu, ambayo hayatoshi kwa wachezaji kurejea katika hali bora,” alisema kocha huyo aliyerithi mikoba ya Youssouph Dabo aliyetimuliwa hivi karibuni.

Kocha huyo aliongeza kuwa wachezaji walionekana kuchoka kutokana na ratiba ngumu ya mechi na kwamba angalau wachezaji wangepata saa 72 kwa ajili ya mapumziko kamili, lakini mara hii hawakupata muda wa kutosha.

“Umeona wachezaji walikuwa wamechoka, walicheza mechi siku mbili zilizopita na hawakuwa na muda wa kutosha kupumzika. Hiyo ndiyo sababu nilifanya mabadiliko,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya wachezaji, Taoussi alisema alifanya hivyo ili kudhibiti sehemu ya kiungo kutokana na kasi ya wapinzani wao wakicheza kwa ukakamavu zaidi katikati, hali iliyowalazimisha Azam kuongeza wachezaji wenye nguvu eneo hiloili kukabiliana nao.

Licha ya uchovu na changamoto za kiufundi, Taoussi alieleza kuwa ana kikosi kipana na aliwaamini wachezaji aliowaanzisha kwenye mechi hiyo.

“Nina kikosi kizuri nje ya uwanja, lakini timu iliyoanza leo ndiyo niliyofanya mazoezi nayo na kuamua ni nani anayeweza kucheza vizuri,” alifafanua.

Ushindi wa bao 1-0 ambao Azam iliupata ni wa pili kwao msimu huu katika ligi, wakiwa chini ya kocha huyo, walianza kwa suluhu dhidi ya Pamba Jiji kabla ya kuitandika KMC kwa mabao 4-0. Matokeo hayo yamewafanya matajiri hao wa Chamazi kufikisha pointi nane wakiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi nyuma ya Fountain Gate (10) na Singida Black Stars (12).