Nne Bara bado hakijaeleweka | Mwanaspoti

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiingia raundi ya sita hadi sasa kati ya timu 16 zinazoshiriki msimu huu ni nne tu ambazo hazijaonja ladha ya ushindi.

KenGold inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa kwanza, kichapo cha juzi cha bao 1-0, ilichokipata kutoka kwa Yanga kimeifanya timu hiyo ya Mbeya kupoteza michezo yote mitano iliyocheza hadi sasa jambo linaloashiria hali ya hatari juu ya mustakabali wa kusalia kama haitagangamala mbele ya safari.

Timu hiyo, ilianza Ligi Kuu Bara na kichapo cha mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, ikachapwa tena 2-1 mbele ya Fountain Gate Septemba 11, ikafungwa bao 1-0 na KMC, kisha kuchapwa na ‘Wanankurunkumbi’ Kagera Sugar 2-0.

Mwenendo huo ni mbaya kwao tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wakati inashiriki Ligi ya Championship ambapo kwa msimu mzima ilikusanya jumla ya pointi 70, katika michezo 30 iliyocheza ambapo ilishinda 21, sare saba na kupoteza miwili tu.

Timu nyingine ambayo haijashinda mchezo wowote ni Coastal Union ambayo msimu huu iliwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kutolewa hatua ya awali na Bravos do Maquis ya Angola kwa jumla ya mabao 3-0.

Coastal inayonolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Joseph Lazaro imecheza jumla ya michezo mitano ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu huku ikiwa haijaonja ladha ya ushindi baada ya kupoteza minne na kutoa sare mmoja tu wa bao 1-1, dhidi ya KMC Agosti 29.

Pamba inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu huu tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, chini ya Kocha Mkuu, Goran Kopunovic, haijashinda pia mchezo wowote hadi sasa kati ya mitano iliyocheza ikitoka sare minne na kupoteza mmoja.

Maafande wa Tanzania Prisons inahitimisha timu nne ambazo hazijashinda hadi sasa ambapo kikosi hicho kinachonolewa na Mbwana Makata, kimecheza michezo minne na kati ya hiyo kimetoa sare yote, kikiwa hakijafunga bao lolote wala kuruhusu.

Kaimu Kocha Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe alisema, ugeni wao katika Ligi Kuu Bara ndio sababu ya wao kupata matokeo waliyonayo kwa sasa, huku Mbwana Makata wa Tanzania Prisons akieleza changamoto kubwa ni kwenye eneo la ushambuliaji.

“Tumeanza vibaya tofauti na matarajio yetu lakini mchezo wetu na Yanga kuna kitu kizuri ambacho wachezaji walikionyesha, nafikiri kama tukiwa na mwenendo huo tunaweza kutoka hapa tulipo leo,” alisema Challe aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu.