Hasheem ndani NBL | Mwanaspoti

LIGI ya Kikapu ya Taifa (NBL) inaendelea katika viwanja vya Chinangali,   mjini Dodoma, lakini kama hujui, kinachonogesha mashindano hayo ni ishu ya usajili.

Mashindano hayo yamevutia mashabiki wengi wa kikapu na zaidi ni kuonekana kwa mastaa wa mchezo huo akiwamo  Hasheem Thabit aliyesajiliwa na Dar City.

Dar City iliyotolewa na JKT katika nusu fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), imeonekana kujiandaa vizuri katika mashindano hayo kutokana na usajili wa wachezaji wengi nyota.

Mbali na Hasheem, wengine waliosajiliwa na timu hiyo ni  Fotius Ngaiza wa Vijana maarufu kama City Bulls, Amin Mkosa anayekipiga Mchenga star, Stanley Mtunguja (Ukonga Kings) na Fadhili Chuma kutoka Uganda.

Wakati huo huo, juzi Fox Divas ya Mara iliifunga Vippers Queens ya Dodoma kwa pointi 75-24 na mchezo wa kwanza iliifunga Orkeeswa kwa pointi 63-22.

Fox Divas ilianza robo ya kwanza kwa uelewano mzuri jambo lililoifanya Vipers Queens kupoteana na iliongoza robo zote nne kwa pointi kwa pointi 30-6, 28-4, 11-8 na 6-6.

Timu zinazoshiriki mashindano hayo upande wanawake ni DB Lioness (Dar), Fox Divas (Mara), JKT Stars (Dar), Orkeeswa (Arusha), Pazi Queens Dar), Vipers Queens (Dodoma) na Vijana Queens (Dar).

Upande wa wanaume ni Eagles (Mwanza), JKT (Dar), TBT (Kigoma), ABC (Dar), Kihonda Hits (Morogoro) na Mvumi Rippers (Dodoma). Zingine ni Dar City (Dar), Kisasa Heroes (Dodoma) na Pamoja BC (Arusha).