Ibenge atenga siku nne Al Hilal ikiifuata Yanga

KIKOSI cha Al Hilal, leo Jumanne Novemba 19, 2024 kimeanza safari kutoka Libya kuja Tanzania kwaajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Novemba 26 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wakati kikosi hicho kikianza safari hiyo, kocha mkuu wa timu hiyo, Florent Ibenge amesema ana siku nne pekee za kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga.

Ibenge amebainisha kwamba, siku hizo nne zimekuja kutokana na kwamba hivi sasa ana wachezaji 13 pekee huku kundi kubwa likiwa na majukumu katika timu zao za taifa kucheza mechi za kuwania kufuzu Afcon 2025.

“Siwezi kusema nimekiandaa kikosi kwaajili ya mechi hiyo (dhidi ya Yanga) kwani huku Libya nilikuwa na wachezaji 13 tu wengine wakiwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa.

“Naweza kusema nina siku nne tu za kukiandaa kikosi changu kikiwa na wachezaji wote,” alisema Ibenge.

Baada ya wachezaji ambao Ibenge anawakosa kipindi hiki cha maandalizi ni Issa Fofana (Ivory Coast), ⁠Jean Claude (Burundi), ⁠Guessouma Fofana (Mauritania), ⁠Yasir Mozamil (Sudan), ⁠Mohamed Abdelrahman (Sudan), ⁠Salah Adel (Sudan), ⁠Ali Abu Ashrin (Sudan) na ⁠Walieidin Khidir (Sudan).

Akizungumzia mabadiliko ya benchi la ufundi la Yanga, Ibenge alisema: “Najua kwamba Yanga imebadili benchi la ufundi lakini ambacho nakiwaza mimi ni kuandaa timu kupata matokeo mazuri ambayo yatatuweka vizuri mapema ili tutafute nafasi ya kufuzu kwenye hatua inayofuata ya mashindano haya.”

Katika safari yao ya kuja Tanzania, Al Hilal ilitoka Mauritania na kuweka kambi ya siku nane nchini Libya na kucheza mechi mbili za kirafiki, moja ikishinda 2-0, nyingine ikitoka suluhu dhidi ya Al Ittihad.

Kutokana na nchini Sudan ligi kusimama kwa muda mrefu kutokana na hali ya kiusalama kutokuwa sawa, Al Hilal kwa sasa inashiriki Ligi Kuu nchini Mauritania ambapo imecheza mechi saba na kushinda tano huku ikipata sare mbili, inaongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa pointi 17.

Yanga na Al Hilal zitakututana katika mchezo huo wa kwanza Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati Al Hilal ikiwa safarini, jana kocha mpya wa Yanga, Sead Ramovic na msaidizi wake, Mustafa Kodro walianza kazi rasmi ya kukinoa kikosi hicho baada ya kuchukua mikoba ya Miguel Gamondi aliyeondoshwa Novemba 15 mwaka huu sambamba na msaidizi wake Moussa N’Daw.

MECHI ZA LIGI ILIZOCHEZA AL HILAL

Inter Nouakchott 1-4 Al Hilal

Al Hilal 2-0 Tevragh-Zeina

Al-Ahly Benghazi 0-1 Al Hilal

Al Hilal 1-1 Al-Ahly Benghazi