MICHEZO miwili ya nusu fainali ya Ligi ya Kikapu Tabora itapigwa keshokutwa (Jumamosi) kwenye Uwanja wa JJ Mkunda Spot Complex na TTC Memphis itaikaribisha Mboka Kings, huku Centre itacheza na Zenga Hawks.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo, Rogers Kitenge alisema timu hizo zimepata nafasi ya kucheza nusu fainali baada TTC Memphis kushika nafasi ya kwanza kwa pointi 10, Centre pointi nane, Zenga Hawks pointi nane na Ukonga kings pointi saba.
Kwa mjibu wa Rogers, nusu hiyo itachezwa kwa timu kucheza michezo mitatu ‘best of three play off’.
“Timu itakayoshinda michezo miwili, itacheza fainali kwa matokeo ya michezo 2-0, “ alisema Rogers.
Wakati huo huo vijana 100 wa umri chini ya miaka 16, wanatarajia kushiriki mafunzo ya mchezo wa kikapu, Desemba 20-24, katika Uwanja wa Lake Side Sport Center.
Akiongea na Mwanaspoti kwa simu kutoka Kigoma, kocha wa timu ya taifa ya vijana na TBT, Anasi Kibonajoro alisema kati yao 50 ni wavulana na 50 ni wasichana na mafunzo yataendeshwa na makocha wenye uwezo mkubwa.
“Tumejipanga kuvumbua vipaji katika mkoa wetu, naamini hadi mwisho wa mwaka 2025, Kigoma utakuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Kibonajoro.