Job, Bocco walivyoupamba usiku wa Madini

NYOTA wengi hawa wa mataifa ya;liyoendelea kisoka wamekuwa wakitumika sana kufanya matangazo na kutangaza bidhaa mbalimbali.

Mbali na matangazo ya picha na video, pia hupita mbele ya majukwaa ya wanamitindo kutangaza bidhaa hizo, kama manukato, mavazi, ujio wa magari mapya, simu, saa na mengine.

wachezaji kama David Beckham, Christiano Ronaldo, Zlatan Ibrahimovic, Hector Bellerin, Fredrick Ljungberg ni mfano tu wa nyota wa soka wanaofanya kazi hiyo na kulamba madili mengi ya aina hiyo kutoka kampuni kubwa.

Kwa hapa Tanzania, ilitokea kwa nyota wawili, Dikson Job wa Yanga na John Bocco wa JKT Tanzania ambao walipata dili hilo sambamba na wanamitindo wengine na wamesema hiyo ni bahati kwao na walipokea mwaliko huo kwa moyo mmoja kwani ni kuitangaza nchi yao.

Ni katika Usiku wa Madini ulioandaliwa Novemba 20, na Wizara ya Madini chini ya Waziri Anthony Mavunde kwa ajili ya kutangaza madini yaliyoko nchini na walipita mbele ya watu waliohudhuria kama wafanyavyo waonyesha mitindo.

wachezaji hao waliungana na wanamitindo wengine kwenye Ukumbi wa Mlimani City kutangaza madini mbalimbali na kuwa kivutio wa waliohudhuria kutoka mataifa mbalimbali.

Baada ya tukio hilo, Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuzungumza na wachezaji nao namna walivyopokea mwaliko huo na walivyoweza kupita mbele za wageni waliohudhuria.

“Kuwa mchezaji mpira sio kwamba unashindwa kufanya vitu vingine, kikubwa ni kujiamini na kujitambua unaweza kufanya kitu chochote ukihitajika, hivyo mimi nilipohitajika kufanya hivi, nikalipokea kwani ni kitu cha kutangaza nchi yetu,” amesema Job ambaye hivi karibuni alikuwepo katika kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu Afcon 2025.

Kwa upande wake Bocco amesema: “Sikuwahi kufanya umodo sehemu yoyote, hii ndiyo mara yangu ya kwanza na kama umeaminishwa unaweza kufanya basi sikusita nikakubali na nikasema nitaweza sababu sikuona ugumu wowote ukizingatia ni jambo la kitaifa.”

Mbali na wachezaji hao, walikuwepo pia  walimbwende Hamisa Mobetto, Miss Tanzania 2024, Halima Kopwe, Miss Grand Fatma Suleiman na wengineo ambao walitumika kunadi madini yapatikanayo Tanzania.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hatua ya kutumia watu hao maarufu ni kutokana na ukweli Tanzania imejaaliwa na utajiri mkubwa ambao mataifa mengine yanapaswa kuwafahamu na kuwavutia kuwekeza nchini kwenye sekta ya madini.

Usiku wa Madini ni mwendelezo wa matukio ya mkutano wa sita wa madini kitaifa na uwekezaji katika sekta ya madini. 

Mbali na shoo ya uanamitindo, kwa upande wa burudani ya muziki ilipambwa na Banana Zorro akiwa na bendi yake ya B Band.