TANZANIA imeibuka mshindi wa pili kwenye mashindano ya Afrika Kanda ya Tatu kwa mchezo wa kuogelea yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Bujumbura nchini Burundi yakishirikisha nchi saba.
Alama 1642 ilizokusanya ndizo zimeifanya Tanzania kushika nafasi hiyo nyuma ya Uganda huku Kenya ikikamata nafasi ya tatu.
Wakati huo huo, Tanzania imetoa mshindi wa jumla kwenye mashindano hayo kwa umri wa miaka 12 wanaume na wanawake ambao ni Nicole Viljoen na Max Missokia aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wanaume na Fidel Kavishe akishika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa waogeleaji wenye umri wa miaka 13 hadi 14, Crissa Dillip ameshika nafasi ya kwanza wanawake wakati Julius Missokia akishika nafasi ya tatu wanaume.
Miaka 15 hadi 16 upande wa wanawake, Filbertha Demello alishika nafasi ya pili huku umri wa miaka 17 wanaume Romeo Mihaly Mwaipasi ameibuka mshindi namba mbili.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Michael Livingstone amewapongeza waogeleaji wake kwa kufanyia kazi maelekezo aliyowapa na kufanikiwa kuibuka washindi wa pili kwenye michuano hiyo.
“Nawapongeza waogeleaji wangu na kwa mmoja mmoja tumefanya vizuri kwa kuibuka washindi kwenye nafasi nyingi,” alisema kocha huyo.