TCB yatoa Sh300 bilioni kuwawezesha Watanzania kukabiliana na mikopo umiza

Dodoma. Jumla ya Sh300 bilioni zimetolewa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa wajasiriamali wadogo tangu mwaka 2023 ilipoanzisha mfumo wa kutoa mikopo kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya mikopo umiza nchini.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Daniel Mbotto ameyasema hayo Desemba 11, 2024 wakati akifungua mkutano wa 57 wa Baraza la Wafanyakazi wa TCB jijini Dodoma.

Amesema miongoni mwa mikakati walioanzisha ni kuanzisha idara ya mikopo ambayo inaangalia mikopo yote inayoanzishwa na ile ya nyuma.

Amesema lengo ni kuhakikisha mikopo inayotolewa ikakuwa bora ambayo inapitia katika mchanganuo kwa kuaangalia iwapo mikopo hiyo italipika kwa kuwa kutakuwa na dhamana ambayo inaweza kufidia ikitokea mikopo hiyo haitafanya vizuri.

“Tunaongea na wateja walioshindwa kulipa mikopo huko nyuma, tunafanya makubaliano walipe kidogo kidogo ama kuuza dhamana walizozitoa ili tuweze kurudisha mtaji wa benki usiteteleke tena na tusirudi nyuma ambapo mtaji wa benki uliondoka kwa sababu hiyo,” amesema.

Amesema tofauti na mikopo kwa ajili ya wafanyakazi wa benki ambayo ina riba nzuri na mikopo inayotolewa kwenye huduma za mitandao kuna mikopo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.

Amesema pia wanatoa mikopo ya kilimo kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambao huwapatia garantii ya mikopo hiyo kabla ya kuitoa.

Amesema mikopo hutolewa kwa riba ya asilimia 9 na 14, riba inayo kutokana na ukubwa wa mkopo.

Amesema yote inafanya mkulima anaweza kupata mkopo kwa bei nafuu zaidi kuliko huko nyuma na hivyo kuwakimbiza wale waliokuwa wakitoa mikopo umiza. Amesema hiyo ndiyo dhamira ya kumfikia Mtanzania.

Kuhusu changamoto ya kuchukua muda mrefu na hivyo baadhi watu kukimbilia katika mikopo umiza, Mbotto amesema kwa wafanyakazi wa Serikali mkopo hutolewa kwa muda usiozidi saa 2.

“Mfumo unasoma unaenda utumishi, unasoma ofisa utumishi anaclick unakuja upande wetu kwa hiyo ndani ya siku hiyo hiyo mtumishi anapata mkopo,” amesema.

Amesema pia wanao mfumo ambao hivi sasa mteja huingiziwa taarifa zote na moja kwa moja makao makuu ya TCB wanaweza kutrack huu mkopo umekwamia wapi na ndani ya siku 14 wanatoa mikopo.

“Ndani ya benki yetu uamuzi unafanyika ndani, tuko karibu na wateja wa kutoa suluhisho kwa haraka zaidi,” amesema.

Aidha, amesema mikopo ya thamani ya Sh300 bilioni imetolewa kwa wajasiriamali wadogo tangu waanze utaratibu huo mwala jana.

“Mikopo hii sio kwa manufaa kwa wenye biashara ndogo bali wanaweza kuajiri watu na kuongeza chachu ya ukuaji wa uchumi katika maeneo yao,” amesema.

Amesema wanaaendelea kutenga na kutoa mikopo ambapo mwaka 2025 watenga na kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa zaidi.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa benki hiyo, Kolimba Tawa amesema katika mkutano huo, wanajadili mpango kazi wa mwaka 2025, bajeti ya mwaka 2025 pamoja taarifa za utekelezaji wa shughuli za mwaka huu.

“Tunachoangalia ni kinachohitajika kufanyika kwa wafanyakazi wote wa benki, wafanyakazi wote wanafanya kitu kimoja, wanakuwa na malengo ya pamoja. Tuna wafanyakazi wa TCB 1,200 lakini hapa tuna wajumbe 70 wanawakilisha wenzao,” amesema.