Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wawekezaji kwa kuwawekea mazingira wezeshi ili kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania.
Amesema takwimu za wahitimu wa vyuo vikuu kwa mwaka 2022 kwa shahada ya kwanza wastani ni vijana 51,000 na hadi kufikia mwaka 2024 inatarajiwa wakafikia zaidi ya 67,000 na wote wanahitaji ajira.
Dk Jafo amesema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa Serikali kutoa ajira, hivyo kinachofanyika inavutia uwekezaji hususani wa viwanda kwa sekta binafsi kuwezesha watu wengi kunufaika.
“Sekta binafsi ndiyo sehemu inayotegemewa kuhakikisha tunatengeneza ajira,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 16, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa mwonekano na chupa mpya ya lita moja ya bidhaa ya African Fruti inayozalishwa na kampuni ya Bakhresa Food Products Limited (BFPL).
“Siku zote mafanikio yanakuja kwa uwekezaji ambao ni sehemu muhimu kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania na kuchangia uchumi wa nchi,” Amesema na kuongeza eneo la viwanda linapewa kipaumbele.
Kupitia uwekezaji na ubunifu uliofanywa na kampuni hiyo inayozalisha bidhaa, zikiwamo zitokanazo na matunda, amesema vijana na wakulima wanapata fursa wanachotakiwa kufanya ni kuongeza uzalishaji wa malighafi.
Ametoa rai kwa wakulima nchini, hasa wa matunda kulima kwa wingi na kuachana na kilimo cha utamaduni, kwani uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji bidhaa za matunda ni mkubwa unaohitaji malighafi hiyo kwa wingi.
“Mnyororo wa thamani kuanzia shambani kwa mkulima, kiwandani hadi kwa mtumiaji wa mwisho unazidi kukua, mmewekeza zaidi ya Sh700 bilioni, mmeweka mashine mpya za kisasa kote huku vijana wameajiriwa,” amesema.
Dk Jafo amesema Serikali inatengeneza mazingira bora kwa wawekezaji kwa kujenga miundombinu ya umeme, barabara na reli akitoa mfano wa treni ya umeme (SGR) ili uzalishaji viwandani uendelee.
“Tukiendelea hivyo tunapata fedha za kigeni, kodi zinalipwa na ajira zinatoka, niwasisitize na kuwahamasisha Watanzania wenzangu tupende vya kwetu, ni jambo la msingi kusaidia uwekezaji,” amesema.
Mkurugenzi Mahusiano Bakhresa Group, Hussein Sufian amesema matumizi ya malighafi za ndani katika uzalishaji wa bidhaa si tu unawanufaisha wakulima na wasafirishaji, bali unaimarisha mnyororo wa thamani na kukuza uchumi wa Tanzania.
“Juisi hii inatengenezwa kupitia matunda yanayozalishwa nchini, tunapobadilisha mwonekano na chupa tumeongeza na ukubwa wa kiwanda kuchakata matunda zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka kutoka tani 45 hadi 50 za sasa,” amesema.
Amesema bidhaa hizo zinachangia kupata fedha za kigeni nchini kwa kuwa zinazalishwa na kuuzwa katika mataifa mengine kama Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Zambia, Sudan, Comoro, Madagascar, Somalia, Malawi, Yemen, China, Mashariki ya Kati hadi Mashariki ya Mbali.
Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika amesema kupitia kampuni za Bakhresa vijana wameanzisha ujasiriamali, ikiwemo uuzaji wa aiskrimu.
“Serikali peke yake haiwezi kutoa ajira kwa watu wote, mnalofanya licha ya kodi mnayolipa, mnatengeza thamani kubwa kwa watu mliowaajiri,” amesema.
Meneja Mkuu wa BFPL, Andanje Mwairumba amesema miongoni mwa athari chanya ni uchumi wa nchi kuongezeka na mnyororo wa thamani kutoka kwa mkulima shambani hadi kwa mtumiaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tetra Pak, Jonathan Kinisu amesema ushirikiano wa kampuni hizo wa zaidi ya miaka 17 unahifadhi mazingira na kuzalisha bidhaa zisizo na kemikali kupitia mitambo ya kisasa.
Mtendaji Mkuu wa kampuni za BFPL, Salim Aziz amesema azma yao inaendana na malengo ya Serikali ya kuzalisha bidhaa za ndani, kuziuza nje na kutoa ajira nyingi zaidi.