Moshi. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema asilimia 10 ya watoto njiti wanaofikishwa hospitalini hapo hufika wakiwa na joto la mwili lililoshuka, hali inayohatarisha usalama wa maisha yao.
Hayo ameyasema leo Jumanne, Desemba 17, 2024 wakati wa kupokea vifaa maalumu vya kufuatilia mwenendo wa hali ya watoto njiti wanapokuwa wagonjwa, vilivyotolewa na Benki ya Maendeleo vyenye thamani ya Sh60 milioni.
Profesa Masenga, amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto hao pindi wanapolazwa katika hospitalini hapo.
Ameongeza kuwa, hospitali hiyo imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 iwe imepunguza vifo vitokanavyo na watoto njiti hadi chini ya 12 kwa kila watoto 1000.
“Hadi hivi sasa, chini ya asilimia 10 ya watoto wanaokuja KCMC wanapata upungufu wa joto la mwili na wengi wao wanatoka nje,” amesema Profesa Masenga.
Naye, Daktari bingwa wa watoto katika hospitali hiyo, Dk Aisiah Shayo amesema kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo utasaidia kuboresha huduma za afya kwa watoto hao.
“Changamoto bado zipo na tunapambana, mara nyingi watoto wanaotoka nje wanakuja na joto la mwili la chini sana na joto la mwili la watoto hao likishuka hata digrii moja, kuna hatari kubwa ya kifo, kwani inaweza kuleta maambukizi ya magonjwa na shida za upumuaji.”
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo, Peter Tarimo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuboresha huduma za afya.
Amesema benki hiyo imefanikiwa kukusanya Sh140 milioni kupitia ushirikishwaji wa jamii na Sh60 milioni kati ya hizo zimeletwa KCMC kununua vifaa vya kusaidia watoto njiti.
“Tutaendelea kuungana na Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa watoto. Ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu,” amesema Tarimo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kuiunga mkono Serikali kwa kutoa misaada katika sekta hiyo ya afya hapa nchini.
Hata hivyo utafiti mpya uliofanywa na Mfuko wa Doris Mollel, unaonesha wazazi nchini hutumia Sh1.3 milioni kumkuza mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati ambaye hakuwa na changamoto yoyote ambayo ni sawa na Sh19,877 kwa siku.