Ulanga. Zikiwa zimepita siku nne tangu mfugaji wa jamii ya kisukuma, Jisandu Mihayo (24) kufariki dunia kwa kinachodaiwa kupigwa fimbo kichwani, mjomba wa marehemu, Donald Paul maarufu, Trump amesema kifo cha kijana wao ni fundisho kwa jamii hiyo ambayo imekuwa ikifanya mchezo swa kuchapana fimbo.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zinadai kuwa Mihayo alifariki dunia Desemba 14, 2024 usiku wakati akipatiwa matibabu katika kituo cha afya Mwaya baada ya kupigwa fimbo kichwani na kijana mwenzake wakati wakicheza mchezo wa jadi wa kuchapana fimbo.
Akizungumza na Mwananchi, Trump amesema mchezo wa kuchapana fimbo ni kawaida kwenye jamii yao, hata wao walipokuwa vijana walicheza na mara nyingi unachezwa jioni wakati wa kutoka machungani.
Hata hivyo, kutokana na kifo cha kijana huyo, wamepata fundisho, baada mazishi watakaa na vijana wao wa kisukuma kuwaonya kuhusu hatari ya mchezo huo.
“Kwa sasa tunaliachia Jeshi la Polisi na Serikali suala la kijana aliyesababisha kifo cha kijana wetu, sisi tunaangalia namna ya kumsitiri kijana wetu na tayari baba yake mzazi tumeshampa taarifa na yupo njiani anakuja kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kwenda kuzika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora,” amesema Paulo.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chiwangawanga, Wilaya ya Ulanga, Thabiti Mpiri amesema taarifa za tukio hilo alizipata saa 12 jioni baada ya kupigiwa simu na mtendaji kata na kuelezwa kuna kijana kapigwa fimbo wakati akicheza na wenzake na akaangua.
“Baada ya kupata taarifa hizo, nilikwenda ofisi ya mtendaji na baadaye polisi kwa lengo la kujua kinachoendelea na muda mfupi kabla sijafika, nilipigiwa tena simu na kujulishwa kuwa kijana amefariki dunia,” amesema Mpiri.
Amesema alikwenda katika kituo hicho kushuhudia mwili wa kijana huyo na baadaye polisi walianza msako wa kumpata mtuhumiwa.
“Polisi waliniomba niongozane nao kwenda kumsaka mtuhumiwa, kutoka pale kituo cha afya Mwaya mpaka kitongoji wanachoishi wafugaji ni zaidi ya kilomita saba tulikwenda na tulifanikiwa kumkamata kijana mmoja kwa tuhuma za mauaji hayo,” amesema Mpiri.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu amepanga kukutana na wafugaji wa jamii ya Kisukuma na Kimasai wilayani humo ili kuzungumza nao na kukomesha mila potofu na michezo ya jadi ambayo imekuwa ikisababisha madhara ya kiafya na wakati mwingine vifo.
“Pamoja na kwamba michezo ya jadi ni moja ya njia ya kuenzi utamaduni wa Kitanzania lakini kama Serikali lazima tuhakikishe inayoleta madhara inakomeshwa,” amesema Dk Ningu.