Raha, karaha twisheni msimu wa likizo

Katika mfumo wa elimu wa sasa, suala la twisheni wakati wa likizo, limezua mjadala mzito nchini Tanzania, huku wadau mbalimbali wakitofautiana kuhusu umuhimu wa muda huu kwa watoto.

Ingawa likizo inapaswa kuwa fursa ya watoto kupumzika na kushiriki shughuli za kijamii, baadhi ya shule zimeonekana kukosolewa na mamlaka kutokana na ufaulu duni wa wanafunzi, hali inayoongeza shinikizo la twisheni kwa shule zinazofelisha.

Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa wakati wa likizo ni wakati wa kupumzika, lakini baadhi ya walimu na wazazi wanadai kuwa kipindi hiki kinatumiwa vibaya, hasa pale walimu wanapojitolea kutoa masomo ya ziada kwa watoto.

Katika baadhi ya shule za Serikali, walimu wanachukua jukumu la kutoa masomo ya ziada ili kuwasaidia wanafunzi kumaliza muhtasari na kufikia malengo ya mitihani.

Hali hii imezua mjadala kama wanafunzi wanahitaji kupumzika au waendelee na masomo ili kuongeza ufaulu.

Mtaalamu wa saikolojia ya watoto kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh, Nikki Miller, anasema twisheni si kwa watoto wanaohitaji msaada wa ziada tu, bali ni kwa kila mwanafunzi anayehamasishwa kuboresha uwezo wake na kujenga ujasiri.

Anasema masomo ya ziada wakati wa likizo yanaweza kusaidia wanafunzi kubadilika kutoka kwa ‘mtoto’ kuwa ‘mwanafunzi’ au kuhamasisha wanafunzi walioko kwenye kiwango cha juu kufikia uwezo wao kamili.

Vita ya likizo na twisheni

Mwaka 2021, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu, alisisitiza kwamba wakati wa likizo, wanafunzi wanapaswa kupumzika na kutoshirikishwa katika masomo ya ziada.

Alisema kuwa, kupumzika ni muhimu kwa afya ya akili ya watoto, kwani walimu wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kufundisha hata wakati wa likizo, jambo linalowachosha wanafunzi na kuathiri uwezo wao wa kujifunza kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa Serikali imepanga vipindi vya masomo vya saa nane kwa siku, na hivyo wanafunzi wanapaswa kutumia muda huu vizuri badala ya kujihusisha na masomo ya ziada.

Hata hivyo, kauli hii ilipokelewa kwa hisia mchanganyiko kutoka kwa wadau wa elimu.

Kauli ya Ummy ilipingwa vikali na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka aliyesema viongozi wakubwa hawajui madhira wanayoyapitia watoto wa maskini, huku akisisitiza kwamba ikiwezekana wakae kabisa kambi wafundishwe kwa kina ili kuomgeza ufaulu.

“Mimi najua watoto wa viongozi wana neema, wanafuatwa na walimu makini nyumbani kwao wanafundishwa na hawasomi shule zenye mazingira magumu kama hizi za kata. Waacheni watoto na walimu wabuni mbinu za kuwasaidia kufaulu,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi na walimu wengi wamepingana na wazo hili la twisheni wakisema kuwa likizo ni wakati mzuri kwa wanafunzi kujipanga na kujiandaa kwa muhula unaofuata.

Mwalimu mmoja kutoka Shule ya Msingi Samuu manispaa ya Shinyanga, anaelezea jinsi masomo ya ziada yanavyosaidia wanafunzi wa shule za Serikali kukamilisha silabasi ambazo mara nyingi huachwa nyuma kutokana na uhaba wa walimu.

Anasema kuwa wakati wa likizo ni muhimu kutumika kumaliza mada ambazo hazijafundishwa ipasavyo, na kuwa hii ni njia bora ya kuongeza kiwango cha ufaulu. “Wanafunzi wanapopumzika muda mrefu, wanapata nafasi ya kuzingatia masomo yao kwa utulivu,” anasema mwalimu huyo.

Anaongeza kuwa wakati wa likizo unapaswa kutumika vizuri na walimu wanapojitolea kutoa masomo ya ziada, wanafunzi wanafaidika kwa kumaliza mada.

Hata hivyo, katikati ya mjadala kuhusu masomo ya zoada wakati wa likizo linaibuka sualala maslahi kwa walimu wanaomenyeka kutekeleza azma hii, huku wengi wakisema kwakuwa wao hawana likizo, hutakiwa kuripoti kazini kama kawaida na kufanya majukumu yote yanayoweza kujitokeza ikiwemo kufundisha twisheni.

Mwalimu mmoja Manisapaa ya Shinyanga ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anasema wanafunzi wameandikiwa kwenye ripoti za matokeo ya muhula wachangie Sh15,000 kwa wiki tatu za mapumziko, fedha hizi ni kwa ajili ya masomo ya ziada, lakini cha kushangaza walimu hufundisha pasipo malipo yoyote kwa kigezo cha kutokuwa na likizo.

“Mimi naona hii pia si sawa, tungegawiwa kidogo kwa sababu huu ni mpango wa biashara nje ya mshahara …kiutaratibu bajeti ya fedha hzi ingekaa ofisi ya mtaaluma na sisi tunaofundisha tukapanga wenyewe, lakini naona wakubwa wanapiga zote…ndio hivyo kaka na ukisema sana mdomo unaweza kusababisha kupoteza kazi,” anasema mwalimu huyo kwa uchungu.

Mmiliki wa shule inayoendesha masomo ya zaida wakati wa likizo anasema: “Walimu wanapaswa kufanya kazi zozote kama hawako likizo ikiwemo kufundisha na kusahihisha kipindi hiki ili kuongeza ufaulu, suala la kuwalipa hilo tunaweza kuwafikiria lakini si haki yao kwa sababu hawako likizo.”

Wanafunzi kutoka shule ya sekondari Chamagua na Uhuru Manispaa ya Shinyanga wanakubaliana na maoni ya walimu wao, wakisema kuwa bila masomo ya ziada, ingekuwa vigumu kwao kufikia viwango vya ufaulu vinavyohitajika.

Wanafunzi hao wanaelezea jinsi walivyokuwa wakichukua juhudi za ziada kwa kujifunza kwa pamoja na walimu hata wakati wa likizo, hasa pale walipokuwa nyuma kimasomo.

“Kwa shule kama yetu, kuna masomo ambayo yalichelewa kufundishwa, na wakati wa likizo ulikuwa ni fursa nzuri kwa walimu wetu kutusaidia kumaliza silabasi,” anasema Brighton Makoye, mwanafunzi wa kidato cha tatu kutika shule ya Sekondari Chamagua.

Wanafunzi hawa wanasisitiza kuwa licha ya kupumzika kuwa muhimu, masomo ya ziada ni muhimu zaidi ili kuwasaidia kufikia malengo yao ya kielimu.

Uzoefu wa twisheni nje ya nchi

Katika muktadha wa Afrika, baadhi ya nchi zimekuwa na mitindo tofauti kuhusu suala la masomo ya ziada.

Kwa mfano, nchini Kenya, masomo ya ziada ni jambo la kawaida, hasa katika shule za umma, ambapo walimu wanachukua hatua za kujitolea kutoa mafunzo ya ziada kwa wanafunzi walio nyuma kimasomo.

Hali hii inatoa fursa kwa wanafunzi kumaliza silabasi na kujipanga kwa mitihani ya kitaifa. Nchini Ghana, shule nyingi zimejizatiti kwa kutoa masomo ya ziada wakati wa likizo, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ufanisi mzuri katika mitihani ya kitaifa.

Hali kama hii inadhihirisha jinsi masomo ya ziada yanavyoweza kuboreshwa, lakini pia inaonyesha changamoto zinazojitokeza kwa shule za Serikali na umuhimu wa kujizatiti kwa walimu.

Kwa upande mwingine, nchi kama Afrika Kusini, imeweka utaratibu wa kupunguza masomo ya ziada na kuzingatia zaidi kupumzika kwa wanafunzi, kwani wanajua kuwa kupumzika ni muhimu kwa afya ya akili ya watoto.

Nchi hii imejizatiti kutoa likizo ndefu kwa wanafunzi, na imekuwa ikijitahidi kutoa mazingira bora ya kujifunza ndani ya darasa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ufanisi bila kuchoka.

Hii inaonesha kuwa suala la likizo ni pana, na linahitaji kufanyiwa kazi kwa umakini ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi.

Kwa hali ilivyo Tanzania, shule za Serikali zinakumbana na changamoto kubwa katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bora, na hili linahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa walimu, wazazi, na serikali.

Shule kama Uhuru na Chamagua zinazidi kuonyesha umuhimu wa masomo ya ziada, lakini pia zinahitaji msaada wa kutosha kutoka kwa serikali ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza.

Hii ni muhimu ili kuzuia wanafunzi kuachwa nyuma kimasomo na kuhakikisha kuwa wanapata matokeo bora katika mitihani ya kitaifa.

Hivyo suala la likizo za wanafunzi linahitaji mjadala mkubwa na ushirikiano kati ya wadau wa elimu.

Walimu wanapaswa kuzingatia usawa kati ya kutoa masomo ya ziada na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata muda wa kupumzika.

Serikali inapaswa kuangalia kwa karibu changamoto zinazokabili shule zake na kutafuta suluhu zinazoweza kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wote.

Wanafunzi wanahitaji kupumzika, lakini pia wanahitaji msaada wa ziada ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu bora.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa viongozi wa elimu kutekeleza sera zinazozingatia haki za watoto, huku wakizingatia umuhimu wa kupumzika na kusoma kwa ufanisi.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.