Tanga. Unamkumbuka yule rais wa ombaomba aliyeshindikana kuondoka Dar es Salaam, hata pale mamlakla zilipomtaka kufanya hivyo?
David Paulo au maarufu kwa jina la Matonya amefariki lakini moyoni hakuwahi kumsahau aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Makamba.
Kwa hakika kama ni mchezo, basi kwa wanaokumbuka ulikuwa wa kuvutia sana kuutazama au kusikiliza. Miamba hii ilisigana hasa na kutunishiana misuli.
Hatahivyo, sikio huwa halizidi kichwa. Mamlaka ni mamlaka. Hatimaye Matonya aliyejiita mtoto wa mjini aliyekuja Dar es Salaam kabla hata ya Uhuru, alisalimu amri.

Akakimbilia mkoani Morogoro alipoendeleza shughuli yake ya kuombaomba. Hata hivyo, unajia ni kwa vipi Matonya aling’oka jijini Dar es Salaam mahala alikopazoea kwa miaka mingi? Fuatana na Mzee Makamba.
Mwisho wa enzi kwa Matonya Dar
Mwananchi limezungumza na Mzee Makamba anayesimulia namna alivyoweza kumuondoa Matonya, licha ya mara kadhaa hatua za kufanya hivyo kufeli.
Anasema aliamua kumfanya rafiki na hata kumwekea fedha katika kopo lake alilokuwa akitumia kuweka fedha anazopewa na wasamaria wema.
‘’Siku moja kwa siri nikaenda alipokuwa analala, nikadondosha sarafu kwenye kopo lake. Zilipolia, akaamka. Hapo nikajitambulisha aliyesimama hapa ni Makamba, Mkuu wa Mkoa, nakutaka uondoke, mkoa huu sio eneo la ombaomba,’’ anasimuliza Mzee Makamba.
Kesho yake, Mzee Makamba alituma timu ya watu kwenda kumhoji Mzee Matonya na ombaomba wengine ili kujua wanatoka kijiji gani na mkoa gani? Mzee Matonya alifichua kuwa alitokaea kijiji kimoja kilichokuwa mkoani Dodoma.
Baadaye anasema aliwasafirisha Mzee Matonya pamoja na ombaomba wengine kwa mabasi zaidi ya 30 kwa ajili ya kuwapeleka mikoa mbalimbali ya Tanzania walipokuwa wakitokea.

Makamba anasema licha ya Matonya kukubali kuondoka Dar es Salaam na kuelekea Dodoma, alilalamika kuwa aliondolewa kinyume cha mapenzi yake, huku akisema anamchukia Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Akimnukuu Matonya, Makamba anasema: ‘’Mimi sijataka kuondoka, Mimi nampenda Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mashishanga (Steven) na naipenda CCM.’’
Licha ya Makamba kufanikiwa kumuondoa Matonya na kumpeleka Dodoma, nguli huyo wa kuomba baada ya mfupi alirudi, lakini safari sio Jiji la Makamba tena bali mkoani Morogoro kwa Mashishanga aliyekuwa anampenda.
Makamba anasema harakati za kusafisha jiji hazikuwa kwa Matonya na ombaomba wengine, bali hata kwa wanawake wanaojiuza.
‘’ Tuliwapeleka polisi na kuwahoji. Nilijitahidi sana kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inakuwa ni jiji la maendeleo na siyo la ombaomba wala changudoa,’’ anasema Mzee Makamba.