Rais wa Kongo afanya mabadiliko makubwa jeshini – DW – 20.12.2024

Mabadiliko hayo yaliyofanywa kwa ngazi mbalimbali, ikiwemo uongozi wa juu wa jeshi na pia kwenye divisheni, yamepokelewa shingo upande na baadhi ya raia wa Kongo.

Wataalamu wa masuala ya jeshi na ulinzi wanadhani, kwamba kuteuliwa kwa Luteni Jenerali Banza Mwilambwe Jules, anaetokea kwenye kikosi cha ulinzi wa rais, kama mtangulizi wake, huenda hapatakuwa na mafanikio zaidi kwenye vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

“Lazima kuweko na maboresho”

Kuna wale wanaodhani kwamba, mabadiliko stahiki,  ni yale yanayoanzia kwenye ngazi za chini na kupanda juu, kama anavyosema Patrick Mundeke, mwanasiasa na pia mchambuzi wa masuala ya ulinzi. 

“Ilikutegemea mabadiliko kwenye uwanja wa mapigano, lazima kuweko na maboresho ya hali ya maisha ya wanajeshi, kuweko na uongozi wa jeshi ulionawatu wenye uzoefu.” 

Kwa upande wake Marrion Ngavo, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Goma, amepokea mabadiliko hayo kwa furaha, huku akiwaomba viongozi wapya wa jeshi, kukomboa maeneo yaliyotekwa na waasi wa AFC-M23. 

“Tunawaomba viongozi wapya wa jeshi wawe wazalendo, wawachukuwe wanajeshi wanaopigana huku mashariki kama watoto wao.”

Ifahamike kuwa, mabadiliko katika uongozi wa jeshi yanafanyika, wakati waasi wa AFC-M23, wanaonekana kusonga mbele kwenye uwanja wa mapambano, katika wilaya ya Lubero, eneo la kaskazini la mkoani wa Kivu Kaskazini.

Juhudi za upatanishi zaendelea

Nchi za magharibi zaendelea na shinikizo dhidi ya viongozi wa Kongo na Rwanda kwa ajili ya kusitisha uhasama
Nchi za magharibi zaendelea na shinikizo dhidi ya viongozi wa Kongo na Rwanda kwa ajili ya kusitisha uhasamaPicha: Arsene Mpiana/Michele Spatari/Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Na huku hayo yakishuhudiwa, Jopo la kimataifa la mawasiliano kwaajili ya nchi za ukanda wa maziwa makuu, linaloongozwa na Uholanzi, limetangaza kuvunjika moyo kutokana na kusuasua kwa mazungumzo ya Luanda, baina ya Rwanda na Kongo.

Katika tamko lao la pamoja lililotolewa jana, Jopo hilo limewaomba viongozi wa Kongo na Rwanda kurudi kwenye meza ya mazungumzo, ili kufanikisha amani ya kudumu katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambao umegeuka kuwa uwanja wa mapambano.

Aidha jopo hilo linalowaleta pamoja wajumbe kutoka Ubelgiji, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani, lilimpongeza rais wa Angola João Lourenço, kwa jitihada zake, ilikuwarudisha tena katika meza ya mazungumzo, viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.