Mwambusi: Dirisha dogo limeshika hatma yetu

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema usajili mzuri watakaoufanya dirisha dogo la usajili utaamua hatma ya timu hiyo ambayo haijawa na matokeo mazuri mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.

Tangu Desemba 15, 2024, usajili wa dirisha dogo umefunguliwa kutoa fursa kwa timu za Ligi Kuu Bara, Championship, First League na Ligi Kuu Wanawake Bara kuboresha vikosi ambapo unatarajiwa kufungwa Januari 15, 2025.

Coastal Union ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 15 za mzunguko wa kwanza ikishinda nne, sare tano na vipigo sita huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu 16.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema amebaini upungufu mwingi kwenye kikosi tangu alipokabidhiwa na tayari ameandaa ripoti na kukabidhi kwa viongozi ili kufanyia kazi. “Sijaanza pamoja na timu nimeingia baada ya ligi kuanza, lakini nimebaini upungufu kwenye nafasi mbalimbali. Nimeandika ripoti na kuhitaji usajili ufanyike ili kuijenga timu ya ushindani ambayo inaweza kupambania pointi mzunguko wa pili,” alisema.

Mwambusi alisema anafurahishwa na juhudi za wachezaji waliopo kuendelea kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na ataendelea kuwajenga ili kuungana na maingizo machache yajayo.