Taoussi amkingia kifua kipa Azam FC

KOCHA wa Azam, Rachid Taoussi amesema makosa yanayoendelea kufanywa na kipa wa kikosi hicho, Mohamed Mustafa ni ya kawaida kwa mtu yeyote, hivyo asingependa kumlaumu nyota huyo zaidi ya kumwambia aongeze umakini katika majukumu yake.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya Mustafa kusababisha bao jepesi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania, kufuatia kushindwa kuudaka mpira vizuri wa frii-kiki uliopigwa na Said Ndemla na kuzaa bao la utangulizi.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Azam ilishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na Pascal Msindo dakika ya 35 na Idd Seleman ‘Nado’ aliyefunga mawili dakika ya 63 na 71, huku la JKT Tanzania likifungwa na Said Ndemla dakika ya 13.

Bao hilo lilisababishwa na madhambi yaliyofanywa na beki wa Azam FC Mkolombia, Yeison Fuentes baada ya kumchezea vibaya, David Bryson na Ndemla kuupiga mpira uliomshinda Mustafa na kuzama wavuni, ikiwa ni mwendelezo wa makosa kwa kipa huyo. “Ni jambo ambalo linaweza kumtokea mchezaji yeyote uwanjani, kuna muda washambuliaji wanashindwa kutumia nafasi, sasa ukitaka kumtupia kila mmoja wao lawama utafeli, kikubwa ninachowasihi ni kuongeza umakini katika michezo tunayocheza,” alisema

Taoussi aliongeza hakuna mchezaji anayeamua kufanya makosa kwa ajili ya kuigharimu timu isipokuwa humtokea kwa bahati mbaya tu, ingawa kwa mwenendo wa washindani wao wanapaswa kuongeza umakini mkubwa ili kutopoteza pointi tena kizembe.

Hiyo ni mara ya pili kwake kufanya makosa baada ya Desemba 13, mwaka huu kusababisha kikosi hicho kupoteza mabao 2-1, dhidi ya Tabora United, huku akisababisha mabao yote mawili yaliyoinyima pointi tatu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Kipa huyo alisababisha mabao hayo akianza kwa kuutokea mpira huku akiwa hana uhakika wa kuudaka na kusababisha bao la kwanza lililowekwa kimiani kwa kichwa na Mkongomani Heritier Makambo, kisha kujifunga mwenyewe la pili na Azam kuchapwa 2-1.

Tangu Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam Septemba 7, mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo aliyetimuliwa Septemba 3, mwaka huu, ameiongoza katika michezo 15 ya Ligi Kuu Bara, akishinda 11, sare miwili na kupoteza pia miwili.

Kwa ujumla Azam imecheza michezo 16, ikishinda 11, sare tatu na kupoteza miwili, ikifunga mabao 25 na kuruhusu manane, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 36, sawa na Yanga iliyopo ya pili ila zikitofautiana tu kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Related Posts