DC aonya watakaovamia Pori la akiba Kilombero

Kilombero. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero (DC), Dunstan Kyobya amesema Serikali haitawafumbia macho watu watakaohusika kudhoofisha jitihada za kulinda na kuhifadhi pori la akiba Kilombero ambalo ni mahususi kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori.

Pori hilo la akiba pia ndio chanzo cha upatikanaji wa maji kupitia mto Kilombero kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika mradi wa kimkakati wa bwawa la Mwalimu Nyerere.

Akizungumzia umuhimu wa kuilinda hifadhi hiyo leo Jumapili, Januari 5, 2025 Kyobya amekemea vikali tabia ya watu wachache wanaowalaghai wananchi walime na kuchunga mifugo ndani ya hifadhi ya pori hilo pamoja na kuwauzia maeneo.

“Imetokea tabia ya watu kwenda kuwashawishi wananchi kwamba maeneo ya hifadhi yanaruhusiwa kulima na kuchunga mifugo, nasema maeneo ya hifadhi hayaruhusiwi kwa shughuli zozote za kibinadamu isipokuwa zile zinazoruhusiwa kisheria.”

“Lakini kuna wengine wanawatapeli wananchi kwa kuwauzia maeneo ndani ya hifadhi ya pori hilo sasa namuagiza OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuendelea kufuatilia kwa ukaribu ili wale wote watakaobainika wanawadanganya wananchi, wanawalaghai, wanawatapeli kwa njia moja ama nyingine wachukuliwe hatua za kisheria,” amesisitiza Kyobya.

Aidha mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa viongozi wa wilaya yake kuongeza ulinzi katika Pori la Akiba Kilombero na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wananchi wanaohama kutoka ndani ya hifadhi hiyo hasa katika maeneo yaliyo pembezoni mwa hifadhi kama vile Mofu, Idete, Mawala, Chombe na Mgeta.

Maeneo mengine aliyoyataja ni pamoja na Chita, kalengakyelu, Chisano Ching’anda, Mlimba, Utengule.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Jamal Idrisa Abdul amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipandisha hadhi pori hilo na kusisitiza kuwa kazi iliyobaki ni kuhakikisha halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) wanalilinda na kulihifadhi sambamba na kurejesha uasili wake.

Mkurugenzi huyo amesema mpaka sasa kazi kubwa wanayoendelea nayo ni kuhakikisha wananchi hawaingii na wala hawaendelezi shughuli za kibinadamu katika hifadhi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa pori hilo, Bigilamungu Kagoma amesema tangu hifadhi hiyo ipandishwe hadhi Tawa imeendelea na shughuli ya uwekaji vigingi ili kuifanya mipaka ya hifadhi kuonekana  na kutambulika vizuri na wananchi, ambapo mpaka sasa zaidi ya vigingi 1,100 tayari vimekwisha wekwa.

Related Posts