Bukombe. “Jana mchana tukiwa darasani mvua ilikua ikinyesha huku kukiwa na radi nyingi, wanafunzi wenzangu wakawa wanapiga kelele nikatoka kwenye dawati nikasogea mbele kufika mbele nageuka nikamuona niliyekuwa nimekaa naye ameungua shingoni na tumboni.”
Haya ni maneno ya Yohana Edward, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Businda aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, baada ya kujeruhiwa na radi iliyopiga kwenye darasa lao na kusababisha vifo vya wanafunzi saba na majeruhi 82.
Tukio hilo lilitokea jana Januari 27,2025 baada ya mvua kubwa iliyoambatana na radi kunyesha wilayani humo wakati wanafunzi wa shule ya Sekondari Businda wakiwa darasani wakiendelea na masomo.
Akizungumza na Mwananchi akiwa amelazwa wodini leo Jumanne Januari 28, 2025, amesema baada ya kuona wenzake wawili wameungua moto chumba cha darasa kilikuwa na harufu kali ya moto wa makuti na moshi ulikuwa umetanda, alianguka chini huku akiendelea kusikia kelele nyingi ambazo hakujua nani anazipiga.
Amesema anachokumbuka alijigusa mgongoni akabaini kuwa anatokwa na damu nyingi.
“Ni kama nilipigwa butwaa siwezi kuongea wala kujisogeza, nikawaona walimu wamefika na kutubeba baada ya hapo nilipoteza fahamu sikujua nini kilichoendelea na nilipozinduka, nikajikuta niko hapa hospitalini,” amesimulia Edward.

Amesema pa moja na kuendelea na matibabu bado ana maumivu karibu mwili mzima.
Mwalimu wa shule hiyo, Shukuru Isack akizungumzia tukio hilo, amesema liliotokea jana mchana wakati walimu wakiwa kwenye kikao ofisini kwa mkuu wa shule.
Amesema taarifa ya wanafunzi kupigwa radi walipatiwa na mwalimu mwingine ambaye aliwafuata kikaoni na kuwaeleza, ndipo wakapiga simu hospitali ya wilaya na baada ya muda mfupi walifika wakiwa na magari.
“Radi hii imepiga kwenye madarasa mawili ambayo ni ya kidato cha tatu B na E, tulipoingia kwenye hayo madarasa watoto walikua kwenye hali mbaya tuliwapeleka hospitali ambapo ilibainika wengine wameshafariki, lakini majeruhi wanaendelea na matibabu,” amesema Mwalimu Isack.
Mwananchi pia imezungumza na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili ambaye amewataja wanafunzi waliopoteza maisha na umri wao kwenye mabano kuwa ni Erick Bugalama (18), Erick Akonay (18), Niacs Paul (17) na Peter Mkinga(18).
Amewataja wengine ni Gabriel Makoye (17) Asteria Mkina (16) na Doto Masasi (17).
DC Muragili amesema kati ya wanafunzi hao waliopoteza maisha, sita ni wavulana na mmoja ni msichana, ambapo tayari Serikali imewasiliana na familia za watoto hao na wataagwa kwa pamoja Alhamisi Januari 30, 2025 katika viwanja vya shule hiyo, ili wenzao sambamba na wananchi, wanafamilia na viongozi mbalimbali washiriki hatua hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela aliyewatembelea majeruhi wa tukio hilo leo na baadhi ya familia zilizopoteza wapendwa wao, amesema Serikali itagharamia mazishi kwa kushirikiana na familia.
“Watoto wetu walioko hospitali watatibiwa na Serikali itabeba gharama, vilevile wale waliopoteza ndugu zao tutazungumza na familia juu ya taratibu za mazishi,”amesema Shigela.
Amesema kati ya majeruhi 82 waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo, tayari 73 wameruhusiwa na tisa wanaendelea na matibabu.
Shigela amesema uchunguzi wa awali umebaini mfumo wa kuzuia radi unaowekwa chini ya ardhi kwenye madarasa yaliyopigwa na radi haukufungwa.
Kutokana na hilo, mkuu wa mkoa amezitaka halmashauri, taasisi zote za umma kwa kushirikiana na wataalamu wa mfumo wa kuzuia radi mkoani humo, kupitia majengo yote na kuhakikisha yanafungwa mfumo wa kuzuia radi na kwa yale yaliyofungwa yaangaliwe kama mfumo bado upo imara, ili kuzuia madhara kama hayo.