UKIZUBAA unaachwa. Ndiyo kinachoenda kutokea kwenye michezo ya robo fainali ya Ligi Daraja la Kwanza Dar es Salaam inayoanza kesho kwenye Uwanja wa Don Bosco, Oysterbay.
Kisasi ni cha Chang’ombe Boys kwa Mlimani B.C baada ya kufungwa katika mchezo wa hatua ya makundi kwa pointi 68-57 na zinakutana tena robo fainali.
Kocha wa Mlimani, Abbas Sanawe anajua Chang’ombe imewapania na amesema watakachofanya ni kupiga kwenye mshono na wasitarajie ushindi kwenye mchezo huo utakaoanza saa 2 usiku.
“Tuliifunga Chang’ombe, kweli tufungwe? Itakuwa ni jambo la ajabu sana,” alisema Sanawe na kuongeza wachezaji wameahidi kuivusha timu kutinga nusu fainali ya ligi hiyo kwani kiu yao ni kufika mbali na hadi BDL.
Katika mchezo huo, Mlimani B.C itawategemea nyota Martine Rogers, Baraka Kweka, huku Chang’ombe itakuwa na Jacobu Marenga, Brando Odhuno na Berry Kankonde.
Mchezo huo utatanguliwa na pambano kati ya Polisi na Yellow Jacket, Stein Warriors na Kigamboni Heroes, Kurasini Heat na Mbezi Beach.
Kurasini Yaitisha Mbezi Beach
Naodha wa Kurasini Heat, Dominic Zacharia amesema timu yake imejipanga kuivuruga Mbezi beach kesho (jumamosi) kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
“Tumejipanga kurudisha heshima iliyopotea miaka mitano iliyopita,” alisema Zacharia na kuongeza nyota wake wote watacheza wakiwamo Daud Daud, Haykal Ibrahim na Anaset maliselo.
Mbezi Beach kushusha vyuma
Wakati Zacharia akiwataja wachezaji wake, Mbezi beach inawategemea nyota wake Adam Ramadhani, Jackson Mrisho, Wilson Maketa na Arnold Harry na wanatarajiwa kuibeba timu hiyo kuibuka na ushindi.