Sudan Kuunda Serikali Ya Mpito Ya Kiraia – Global Publishers



Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza mipango ya kuunda serikali ya mpito. Katika hatua nyingine, wizara hiyo pia imetangaza na kufafanua kuwa jeshi linapanga kurejesha utawala wa kiraia baada ya kupata udhibiti wa maeneo kadhaa kutoka Rapid Support Forces (RSF)
Mpango huo, unaosimamiwa na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, unajumuisha kuunda serikali ya mpito, kuteua waziri mkuu wa kiraia, na kuanzisha mazungumzo ya kitaifa.

Jeshi linadai kuwa limepata mafanikio katika maeneo ya Khartoum, Sennar, Gezira, na Kordofan Kaskazini, huku RSF ikiendelea kudhibiti maeneo mengi ya Darfur na Kordofan Magharibi. Wizara hiyo imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa—ikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu—kuuunga mkono mpango huo kwa lengo la kuleta utulivu na demokrasia nchini Sudan. Huku hali ya kibinadamu ikizidi kuzorota, jumuiya za kimataifa zinakabiliwa na changamoto kubwa za kusaidia mamilioni ya Wasudan wanaohitaji misaada ya haraka.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan wameripoti kuwa vikosi vya wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) vinazuia misaada ya kuokoa maisha kuwafikia watu wanaohitaji zaidi katika mkoa wa Darfur, ambao umekumbwa na baa la njaa.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF yalianza Aprili 2023, na yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 28,000 huku mamilioni wakilazimika kuyakimbia makazi yao.