Mbeya. Wagonjwa wa saratani wamesema kutokana na gharama kubwa matibabu husabaisha kukatisha tamaa, huku wengine kuamua kukimbilia kwenye maombi na kwa waganga wa kienyeji wakiomba Serikali kuona namna ya kupunguza gharama ili kuokoa maisha.
Wakizungumza leo Jumatano, Februari 12, 2025 baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Mbeya kutoa msaada wa vifaa tiba kwa wagonjwa hao, wamesema gharama za matibabu ni kubwa hali ambayo inawakatisha tamaa.
Maria Ambilikile amesema katika mizunguko nane ya matibabu, mzunguko mmoja hugharimu Sh1.8 milioni hali ambayo kwa kipato cha mwananchi wa kawaida ni ngumu sana kukifikia.
Amesema wanaomba Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona uwezekano wa kupunguza gharama kwa kiasi atakachopendezwa ili kumsaidia mgonjwa kuweza kumudu gharama hizo.
“Tunashukuru TRA kwa msaada huu, ugonjwa huu ni gharama kubwa kuukabili ambapo mzunguko mmoja tu ni Sh1.8 milioni, binafsi nilifika hatua nikamwambia daktari kwamba inatosha nasubiri muda wangu nife nipumzike,” amesema.
“Siwezi kumpangia Rais apunguze kiasi fulani, bali yeye atajavyopendezwa kwakuwa hali yetu wengine ni ngumu kukamilisha matibabu haya” amesema Maria.
Kwa upande wake Alfao Mbunju amesema kutokana na gharama kubwa baadhi hukata tamaa na badala yake huamua kukimbilia kwenye maombi na muda mwingine kwa waganga wa kienyeji kupata tiba na mwisho hupoteza maisha.
Amesema ikiwa mwaka wa tano akiunmguza ugonjwa huo, mzunguko mmoja alitumia Sh1.6 milioni akieleza kuwa ugonjwa huo hautafutwi bali ni bahati mbaya kumkuta yeyote akiomba Rais kupunguza gharama au kutoa bima.
“Ni ugonjwa unaotutesa sana, gharama zake ni kubwa mno, wengine wanaamua kwenda kwenye maombi na kwa waganga wa kienyeji, Rais atusaidie aidha bima za afya au atupunguzie gharama, wengine tunasikia wamekufa mtaani,” amesema Mbunju.
Daktari bingwa wa magonjwa hayo katika Hospitali ya Kanda Mbeya, Dk Irine Nguma amesema idadi ya wagonjwa ni kubwa na inazidi kuongezeka kutokana na mfumo wa maisha haswa uvutaji sigara, pombe na ngono zembe.
Amesema kutokana na msaada huo kutoka TRA utaenda kusaidia kwa muda huu ambao wagonjwa wakiendelea kupata matibabu hospitalini hapo akikiri kuwa gharama ni kubwa kwani wapo wanaotoka nje ya Mbeya.
“Kwa mwaka tunahudumia wagonjwa zaidi ya 900 wa saratani, idadi ni kubwa na itazidi kuongezeka kutokana na mfumo wa maisha ikiwamo matumizi ya pombe, uvutaji sigara na ngono zembe, tujitahidi kufanya mazoezi,” amesema.
“Saratani inashika jinsia zote wanaume, Wanawake na watoto, ambapo saratani ya mlango wa kizazi ndio inaongoza ikifuatia ya matiti na Wanawake ndio wanaoathirika zaidi hivyo tunawashauri wakafanye vipimo vya mara kwa mara,” amesema Dk Irine.
Akielezea msaada huo, Meneja Idara ya Upelelezi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Nyanda za Juu Kusini Nicholaus Njovu amesema lengo ni kurudisha shukrani kwa walipa kodi na kwamba wao kama sehemu ya Watanzania wanaguswa na maeneo yote.
Amesema kodi za wananchi zinalenga kuboresha miundombinu mbalimbali ya maendeleo ikiwamo barabara na sekta ya afya, hivyo msaada wa vifaa hivyo ikiwamo dawa itasaidia kwa kiasi fulani wagonjwa hao.
“Tulipokea maombi ya msaada kutoka hospitali hii, japo mahitaji tuliona yapo kwa wagonjwa wa saratani hivyo msaada huu wa vifaa tiba na dawa vya Sh5 milioni vitasaidia, haya ndio malengo ya kodi ya wananchi kugusa maeneo yote,” amesema Njovu.