Rais Donald Trump amefanya tukio adimu la kujitokeza hadharani pamoja na mshauri wake mwenye ushawishi mkubwa, Elon Musk, katika Ofisi ya Oval, Ikulu ya White House jana Jumanne, Februari 11, 2025, kabla ya kusaini amri nyingine ya kiutendaji mbele ya waandishi wa habari ya kuendeleza juhudi zao za kupunguza idadi ya wafanyakazi wa serikali kuu na kuwaondoa wengine.
Musk aliambatana pia na mtoto wake wa kiume, Lil X.
Musk, ambaye amekuwa mshauri wa karibu wa Rais Trump, alieleza kuwa wafanyakazi wa serikali ni kama tawi la nne la serikali lisilo la kuchaguliwa, ambalo linapaswa kuwajibishwa.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Musk kujitokeza hadharani tangu alipoteuliwa kuongoza Idara mpya ya Ufanisi wa Serikali, ambayo yeye na wafanyakazi wake wanadaiwa kuiendesha kwa usiri mkubwa bila uwajibikaji wowote.
Hata hivyo, alipoulizwa na wanahabari waliokuwa wamejazana ofisini humo kuhusu madai hayo, Musk alikanusha vikali na kueleza kazi ambayo imeshafanywa na idara yake hiyo.
Rais Trump alisaini amri ya kiutendaji inayolenga kupunguza ajira na matumizi ya serikali kuu, isipokuwa katika sekta zinazohusu uhamiaji, utekelezaji wa sheria, na usalama wa umma.
Siku ya Jumatatu, Februari 10, 2025, Mkaguzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) alitoa onyo kwamba kuvunjwa kwa USAID na utawala wa Trump kumeifanya iwe vigumu kufuatilia matumizi ya dola bilioni 8.2 (sawa na shilingi trilioni 21.13 za Kitanzania) zilizotengwa kwa misaada ya kibinadamu.
Hata hivyo, siku iliyofuata, Jumanne, Februari 11, Ikulu ya White House ilimfukuza kazi mkaguzi huyo bila kutoa sababu wala maelezo yoyote.
Kesi mpya iliyowasilishwa mahakamani inadai kuwa kufungwa kiholela kwa USAID kumeziacha biashara za Marekani bila kulipwa mamia ya mamilioni ya dola kwa kazi ambayo tayari ilikamilika.
Rais Trump ameonekana kumuamini na kumtegemea sana bilionea Elon Musk katika uendeshaji wa serikali, jambo ambalo limeibua mjadala mkali na ukosoaji kutoka kwa wachambuzi wa siasa kuhusu mustakabali wa uongozi wake katika awamu yake hii ya pili.