Chama Cha Mapinduzi kimesema kitamtambulisha mgombea urais wa Zanzibar wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Pemba.
Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amesema Dk Mwinyi atatambulishwa Februari 15 mwaka huu katika visiwa hivyo.
Mbeto alielezea taratibu zitakazotumika katika mapokezi ya mgombea mteule wa urais wa Zanzibar ,kwa tiketi ya CCM, atakaewasili Pemba na kutambulishwa kwa wana CCM.
“Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi atawasili Pemba na kutambulishwa kwa wana CCM wenzake. Wakati wa kumtambulisha mbele ya wananchi haujawadia. Anakuja ili kupongezwa na wana CCM kwa kuteuliwa,” alisema mwenezi huyo.
Vilevile Mbeto amewatolea wito wana CCM katika Mikoa miwili ya Pemba, Kusini na Kaskazini, kujitokeza katika ofisi za CCM ili kumlaki mgombea huyo mteule wa urais mwaka 2025.
Akizungumzia wapiga kura Mbeto alisema kila Mtanzania iwe amezaliwa Zanzibar, Mwanza , Mkokotoni , Mtwara, Mkanyageni au Katavi hawezi kupiga kura Zanzibar bila kutimiza vigezo vilivyotajwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha kwa matakwa ya katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, mpiga kura kwanza awe Mzanzibari aliyeishi jimboni miezi 36 ikiwa mzaliwa wa Tanzania Bara aishi Zanzibar miaka kumi pia awe mkaazi wa shehia husika kwa miezi 36.
Mbeto alieleza hayo alipozumgumza na waandishi wa habari huko Chachani Wilaya ya Chake Chake Mkoa Kusini Pemba.
Alisema haki ya kupiga kura haitokani na mtu kuwa na cheti cha kuzaliwa Zanzibar, kuwa na Kitambulisho cha Mzanzibari, Mkaazi au Kitambulisho cha uraia wa Mtanzania.
Alisema mwananchi yeyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye kitambulisho cha Taifa cha uraia pia kuwa mzaliwa wa Zanzibar, ana haki kuwa na vitambulisho vya Zanzibar (ZAN ID) na kwa Mtanzania mwenye Kitambulisho cha Taifa (TAN ID), hivyo bado si vigezo vya kuwa mpiga kura.
Alisema baadhi ya watu kwa nia ovu hupotosha sheria na matakwa ya katiba ili kufikia matakwa yao kisiasa, kinyume na katiba na kudai kuna watu wanakataliwa kuandikishwa kwenye Daftari la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).