India Kuwekeza Katika Sekta Ya Nishati Nchini – Global Publishers


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Hardeep Singh kuhusu nia ya nchi hiyo kuzidi kuimarisha biashara kati yake na Tanzania kupitia sekta binafsi, kufanya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati na kujengea uwezo wataalam.

Mazungumzo hayo yamefanyika Februari 11, 2025 jijini New Delhi nchini India katika Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati nchini humo.

Dkt. Doto Biteko amemweleza Waziri Singh kuwa milango ya uwekezaji Tanzania ipo wazi na kampuni mbalimbali kutoka India zinaweza kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya umeme, usambazaji wa gesi ya mitungi (LPG) na uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Bulk procurement) kwani kunahitajika washindani wengi ambao watatoa uhakika wa uwepo wa mafuta wakati wote.

“ Tanzania tumejikita katika kuhakikisha tunatumia kila rasilimali tuliyonayo ili kuwa na nishati ya kutosha ikiwemo umeme ili kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, ameeleza kuhusu umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza miradi mbalimbali akitolea mfano kuwa, ili Tanzania ijitosheleza kwa mahitaji ya nishati inahitaji Dola za Marekani Bilioni 12 ambazo kupatikana kwake lazima sekta binafsi ihusishwe hivyo kupitia kwa Waziri Singh, amekaribisha wawekezaji kutoka India kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati nchini.

Kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Nishati India amesema kuwa Tanzania imefaidika na ushiriki wake katika Wiki hiyo kwani India tayari imeshapiga hatua kwenye Sekta ya Nishati hivyo imekuwa ni sehemu maalum ya kujifunza zaidi kuhusu sekta, kubadilishana uzoefu na kunadi fursa za uwekezaji ikiwemo duru ya tano ya uendelezaji wa visima vya mafuta na gesi asilia Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh amesema kuwa India ina uhusiano mzuri wa kibiashara na Tanzania ambapo biashara kati ya pande hizo mbili imezidi kuimarika na kueleza kuwa nchi hiyo imejipanga kuimarisha zaidi biashara yake kwa Tanzania.

Related Posts