Urusi Yajibu Vitisho Vya Trump Dhidi Ya BRICS – Global Publishers



Rais Donald Trump wa Marekani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imetoa taarifa kuhusiana na tishio la Rais Donald Trump wa Marekani la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za BRICS iwapo dola itafutwa katika mabadilishano ya kibiashara ya nchi hizo.Urusi imesisitiza kuwa ushirikiano wa nchi wanachama wa BRICS unalenga kuimarisha uwezo wa kijamii, kiuchumi na kibinadamu wa nchi hizo.

Rais Trump mwenye utata mwingi, alitangaza Januari 30 mwaka huu kwamba Marekani itatoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa kutoka nchi za BRICS ikiwa kundi hilo litatumia sarafu nyingine isiyokuwa dola katika biashara zake za kimataifa. Amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusu dola kutelekezwa katika biashara ya kimataifa na kuonya kuwa nchi zitakazofanya hivyo zitakabiliwa na hatua kali za kibiashara kutoka Marekani.

Katika kujibu tishio la Trump, Dmitry Peskov, Msemaji wa Ikulu ya Urusi Kremlin, ameashiria matamshi ya Rais Vladimir Putin wa Russia, ambaye awali alisema kuwa hakuna mipango yoyote ya kuunda sarafu ya pamoja katika kundi la BRICS, na kwamba limeazimia kuunda majukwaa mapya ya uwekezaji ambayo yataruhusu uwekezaji wa pamoja katika nchi za upande wa tatu.

Desemba 2024, na katika kukabiliana na tishio la Trump la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za BRICS, Putin alibainisha kuwa kutokana na vitendo vya Wademocrat, dola haina tena nguvu iliyokuwa nayo miaka minne iliyopita wakati wa urais wa kwanza wa Trump.