Hospitall ya Mount Meru kuwatibu wagonjwa majumbani

Arusha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, itaanza kutoa huduma ya matibabu kwa kuwafuata nyumbani wenye magonjwa ya muda mrefu, magonjwa sugu kama saratani na wenye changamoto za kiharusi.

Huduma hiyo ambayo inatarajia kuanza kutolewa Oktoba mwaka huu, tayari Serikali imewekeza zaidi ya Sh300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, Dk Alex Ernest akitoa taarifa ya utekelezaji wa hospitali hiyo jana amesema umelenga wagonjwa wengine.

“Wengine ni wale wenye vidonda vya muda mrefu vinavyohitaji uangalizi hasa vinavyosababishwa na ugonjwa wa kisukari,” amesema.

Amesema utaratibu huo umelenga kupunguza gharama za kuhudhuria hospitali kwa wagonjwa hao.

Dk Ernest pia amesema lengo lingine ni kuwaepusha wagonjwa hao na changamoto zinazoweza kujitokeza barabarani wakati wa kwenda na kurudi hospitali.

Akitaja sababu za kuanzisha huduma ya tiba majumbani, amesema imetokana na walivyoshuhudia namna wagonjwa wanavyopata shida kuhudhuria hospitalini kupata huduma huku wakihitaji msaada wa ndugu ambao nao wanaingia kwenye gharama kubwa ya usafiri.

“Tulikaa tukaona shida hiyo na tukagundua kuwa kuliko waje waunge foleni na wakumbane na changamoto mbalimbali barabarani bora sisi tuwafuate huko nyumbani kwa gharama ndogo watakayokuwa wanachangia” amesema.

Amesema huduma hiyo itaanza kutolewa Oktoba mwaka huu baada ya kukamilisha maandalizi ya utoaji wa huduma hiyo ikiwemo ununuzi wa vifaa.

“Tayari tumeshaandaa wataalam na wabobezi wa huduma hizo na pia Serikali imewekeza zaidi ya Sh300 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na taratibu zimeshaanza kwa ajili ya kuletwa hapa hospitalini vianze kazi yake mara moja” amesema Dk Ernest.

Mbali na hilo Dk Ernest amesema, hospital hiyo imeanzisha program ya simu (app)  iliyopewa jina la ‘Mount Meru afya yangu’ kwa ajili ya kusaidia wananchi kupata elimu ya afya zao mara kwa mara, lakini pia kujua taarifa za magonjwa kwa lengo kujua kinachomsumbua kabla ya hata ya kwenda hospitali.

“Programu hiyo ambayo tumeanza kufanyia majaribio tutaiachia hivi karibuni kwa ajili ya kusaidia wananchi wetu kujua wanachoumwa, lakini pia anaweza kuongea na madaktari wetu na kupata ushauri kwa urahisi.

“Kama ataonekana anatakiwa kuhudhuria hospitali kwa ajili ya vipimo au ushauri zaidi anaweza kuweka ahadi na daktari husika hapo hapo badala ya kuja hapa kuunga foleni na kupoteza mda” amesema Dk Ernest.

Dk Ernest amesema kuwa tatizo kubwa linaloonekana kuwasumbua kwa Mkoa wa Arusha ni magonjwa yasiyoambukiza ambapo kwa miezi mitatu pekee tangu Oktoba hadi Desemba mwaka jana wamepokea jumla ya wagonjwa 1,485 waliokutwa na kisukari na 1,173 walikutwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu (presha).

“Magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza yamekuwa tatizo kubwa kwa Arusha na hii inatokana na mtindo mbaya wa maisha hasa ulaji mbovu na kutofanya mazoezi hivyo nitumie nafasi hii kuwahamasisha wananchi wazingatie mtindo mzuri wa kula na kufanya mazoezi,” amesema.

Kuhusu msahama kwa wagonjwa wenye changamoto za kiuchumi, Dk Ernest amesema katika kipindi cha miezi mitatu pekee, wametoa msamaha wa takriban Sh82.62 milioni kwa wagonjwa ambao wamehudhuria hospitalini hapo na kupata matibabu ambayo wameshindwa kulipia.

“Hiyo ni kwa miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba ambayo baadhi ya wagonjwa wanakuja kutibiwa na mwisho wa siku wanapewa bili lakini wanashindwa kulipia na wanabainika kweli hawana uwezo wa kulipa kupitia kitengo chetu cha ustawi wa jamii tunaamua kuwasamehe” ameongeza Dk Ernest.

Mmoja wa wanawake waliokuja tibiwa katika hospital hiyo, Merry Samwel amesema maboresho ya majengo, huduma na miundombinu katika hospitali hiyo ni makubwa na kuiomba uongozi kuzingatia weledi na maadili ya wahudumu wao.

“Mfano sisi wa kujifungua maboresho ni makubwa tangu nimejifungua mtoto wangu kwa kwanza mwaka 2002… mabadiliko ni makubwa, lakini baadhi ya wahudumu sijui ni kuchoka au wito hawana wamekuwa hawajali kabisa mgonjwa anapolalamika kuzidiwa uchungu hali inayohatarisha maisha ya wanawake wengi na watoto wanaotarajia kuwazaa” amesema.