Rais wa Marekani Donald Trump aliyeahidi kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine sasa ameanza kufanyia kazi ahadi hiyo.
Jana Februari 12 Trump amefanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladmir Putin juu ya kusimamisha vita vinavyoendelea baina ya nchi yake na Ukraine.
Kupitia mtandao wake wa Truth Trump rais huyo wa Marekani ameandika “Nilikuwa na mazungumzo marefu na yenye tija kubwa kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa Urusi. Tulijadili kuhusu kumaliza vita ya Ukraine, Mashariki ya Kati.
“Tumejadili kuhusu nishati, akili mnemba, nguvu ya Dola ya Marekani, na masuala mengine mbalimbali. Lakini kwanza, kama tulivyokubaliana, tunataka kusitisha vifo vya mamilioni ya watu vinavyoendelea katika vita vya Urusi na Ukraine.”
Trump ameeleza kuwa yeye atampigia simu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kumpa taarifa juu ya mazungumzo yake na Putin kisha baada ya hapo hatua ya mazungumzo ya kusitisha vita itaanza rasmi ambapo wameunda timu kwa pamoja zitakazoongoza majadiliano hayo mara moja.
Aidha Trump ameongeza kuwa watashirikiana kwa karibu sana na Putin, ikiwa ni pamoja na kutembeleana katika mataifa yao.