Papa Francis Apelekwa Hospitali, Chanzo Chatajwa – Global Publishers


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, alikimbizwa hospitali ya Policlinico Agostino Gemelli mjini Roma jana Ijumaa, Februari 14, 2025, kutokana na ugonjwa wa mapafu unaomsumbua. Vatican ilitangaza kuwa Papa atalazimika kusitisha matukio kadhaa yaliyoratibiwa kwa siku tatu zijazo.

Taarifa ya Vatican ilieleza: “Papa Francis amelazwa katika Hospitali ya Policlinico Agostino Gemelli kwa vipimo vya uchunguzi na kuendelea na matibabu ya ugonjwa huo (bronchitis) katika mazingira ya hospitali.” Hii inafuatia kipindi cha zaidi ya wiki moja ambapo Papa amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo.

Kutokana na hali yake, Vatican imetangaza kuwa hatashiriki katika Misa ya Jumapili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Aidha, mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika Jumamosi na ziara yake kwenye studio maarufu za filamu za Cinecitta mjini Roma Jumatatu, pia zimefutwa.

Papa Francis amekuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya kwa muda mrefu. Akiwa kijana, alipata maumivu ya kifua yaliyosababisha kuondolewa sehemu ya moja ya mapafu yake, na hivi karibuni amekuwa akipata maambukizi ya mapafu mara kwa mara. Mapema mwezi huu, aliwaambia mahujaji katika mkutano wa kila wiki kuwa alikuwa na “mafua makali,” hali ambayo Vatican baadaye ilithibitisha kuwa ugonjwa wa mapafu (bronchitis).

Licha ya changamoto hizi za kiafya na kupungua kwa uwezo wa kutembea, Papa Francis ameendelea kuwa na ratiba yenye shughuli nyingi, ikiwemo safari za nje ya nchi. Mnamo Septemba 2024, alimaliza ziara ya siku 12 barani Asia Kusini-Mashariki na eneo la Oceania, ambayo ilikuwa safari ndefu zaidi katika uongozi wake.

Hadi sasa, hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu hali ya afya ya Papa Francis, na waumini kote duniani wanaendelea kumuombea apate nafuu haraka.