Trump Atangaza Kukutana Na Putin – Global Publishers

Rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Jumapili jioni kuwa atakutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika siku za usoni. Trump anaamini kuwa Putin ana nia ya dhati ya kusitisha mapigano nchini Ukraine. Hata hivyo, hakutaja tarehe maalum ya mkutano huo.

Kauli hiyo ya Trump imetolewa saa chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kuanza ziara yake jijini Riyadh, Saudi Arabia. Rubio atakutana na viongozi wa Urusi kujadili namna ya kumaliza mzozo wa Ukraine, ambao unakaribia kutimiza miaka mitatu.

Trump amesema kuwa timu yake imekuwa ikiwasiliana kwa muda mrefu na maafisa wa Urusi, akiwemo mjumbe wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff. Kwa mujibu wa Trump, Witkoff alikutana na Putin hivi karibuni kwa takriban saa tatu.

“Nadhani Putin anataka kusitisha vita, na ikiwa angeendelea, hilo lingenisababishia tatizo kubwa,” alisema Trump. Alipoulizwa ikiwa anaamini kuwa Putin anataka kuichukua Ukraine yote, Trump alijibu: “Hilo lilikuwa swali langu kwake.”

Trump alisisitiza kuwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, pia anataka vita vimalizike haraka.

Hata hivyo, mataifa ya Ulaya yamekosoa juhudi za Marekani za kuongoza mazungumzo ya amani bila ushirikiano wao. Waziri Rubio amesema kuwa nchi za Ulaya na Ukraine zitajumuishwa kwa wakati muafaka kwenye mchakato huo.

Related Posts