Benki ya
Exim Tanzania imeimarisha dhamira yake ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii
Zanzibar kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta hiyo, wakiwemo Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili
kuwezesha waendeshaji wa shughuli za utalii kufanya malipo kama ada za kuingia
kwenye hifadhi kwa haraka, kwa usalama na kwa urahisi. Mkutano wa Z-Summit
2025, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Tunguu, uliwakutanisha wadau wa
serikali, wafanyabiashara, na wadau wa sekta ya utalii na ukarimu ili kujadili
suluhisho bunifu za kuboresha nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya
utalii duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim,
Shani Kinswaga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisisitiza
safari ya benki hiyo na Z-Summit tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa huu ni
mwaka wa tatu mfululizo wa udhamini wao katika mkutano huo.
“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kushirikiana, kubadilishana maarifa na
kujadili mikakati ya kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora
vya utalii duniani. Uungwaji mkono wa Benki ya Exim unaonesha imani yetu
thabiti katika sekta ya utalii kama kiini cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa
jamii,” alisema Kinswaga.
Kinswaga alielezea juhudi za benki hiyo katika kutumia teknolojia kutoa
suluhisho rahisi za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara za utalii. Kwa
kuongezeka kwa mahitaji ya miamala ya kidigitali, Benki ya Exim imeanzisha
huduma bunifu za kibenki, zikiwemo kutumia simu, kadi, na mifumo ya malipo
mtandaoni, ili kuhakikisha ufanisi, usalama, na urahisi kwa wafanyabiashara na
watalii.
Akizungumzia ushirikiano wao na TANAPA, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha
Benki ya Rejareja wa Benki ya Exim, alisema, “Katika Benki ya Exim, tunatambua
kuwa ufanisi, usalama, na urahisi ni muhimu katika sekta ya utalii. Ndiyo maana
tumeshirikiana na wadau kama TANAPA na NCAA kuwezesha malipo yasiyo ya fedha
taslimu kwa huduma mbalimbali, ikiwemo ada za kuingia kwenye hifadhi. Akaunti
ya Waendeshaji wa shughuli za Utalii inajumuisha Kadi ya Exim TANAPA,
iliyoundwa mahsusi kurahisisha miamala katika maeneo yote ya hifadhi nchini
Tanzania.”
Katika kuthibitisha dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za
kifedha, Benki ya Exim ilitangaza mpango wake wa kuendelea kupanua huduma zake
Zanzibar. Ikiwa tayari na matawi mawili yanayofanya kazi, benki hiyo ina mpango
wa kufungua matawi katika maeneo mengine ya kimkakati. Hii inaonesha azma ya
Benki ya Exim ya kusogeza huduma za kibenki karibu na biashara, ikiwawezesha
kupata suluhisho za kifedha zinazosaidia maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa
biashara, na ufanisi wa uendeshaji.
Kadri mazingira ya utalii yanavyoendelea kubadilika, Benki ya Exim
inasalia kuwa mshirika wa kuaminika wa kifedha kwa biashara zinazotaka
kupanuka, kuboresha huduma zao, au kuwekeza katika fursa mpya. Suluhisho zake
maalum za kifedha zimeundwa kusaidia kupata rasilimali zinazohitajika ili
kustawi katika soko lenye ushindani.
Kupitia ushirikiano imara, matumizi ya teknolojia za kidigitali, na
upanuzi wa huduma zake, Benki ya Exim haitoi tu msaada kwa sekta ya utalii bali
pia inachangia katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.
Ushiriki wa Benki ya Exim katika mkutano wa Z-Summit 2025 ni uthibitisho
wa dhamira yake isiyotetereka ya kusaidia ukuaji endelevu wa sekta ya utalii
Zanzibar. Kwa kushirikiana na wawekezaji, wafanyabiashara, na mamlaka za
serikali, benki hiyo inaunda mustakabali ambapo utalii utaendelea kuwa
kichocheo cha maendeleo ya uchumi, kuongeza ajira, na kuifanya Zanzibar kuendelea
kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka kote ulimwenguni.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mh. Mudrick Soraga (kulia), akimsikiliza Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shani Kinswaga, wakati wa kongamano la Z-Summit 2025 lililofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Zanzibar. Kongamano hilo la kila mwaka, lililofanyika kuanzia Februari 19-20, liliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ili kujadili changamoto na suluhisho za kuendeleza Zanzibar kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani.