MBUNGE WA MADABA AAHIDI UJENZI WA MRADI WA MAJI KUKAMILIKA KARIBUNI KIJIJI CHA NGADINDA KATA YA GUMBIRO

 Na Belinda Joseph, Ruvuma.

Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Kizito Mhagama, amewataka Wakazi wa Kijiji cha Ngadinda Kata ya Gumbiro Halimashauri ya Madaba, kuwa na subra wakati mradi wa maji safi na salama ukiwa mbioni kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa jamii siku za hivi karibuni ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kwa wananchi kuhakikisha anasimamia na  kufikisha huduma hiyo kwenye Kijiji hicho.

Akizungumza katika ziara yake ya kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mbunge huyo amesema kuwa mradi huo uko katika hatua za mwisho kukamilika na kwamba hivi karibuni ndani ya wiki 2  kazi ya kuchimba mitaro na kufukia mabomba itaanza.

“Mradi huu umegharimu zaidi ya Bilioni 1 na Milioni 300 na tuko katika hatua nzuri, Tunawaomba wananchi waendelee kuwa na subira wakati kazi ya ujenzi ikiendelea, kwa sababu tuna malengo ya kuwanufaisha kwa huduma ya maji safi na salama,” alisema Mbunge huyo.

Mbunge huyo pia amekiri changamoto wanazozipata kinamama katika kutafuta maji, huku akiwahidi wakazi wa Kibaoni kuwa hivi karibuni watachimba kisima kirefu kitakachowasaidia katika shughuli za kilimo hususan katika uzalishaji wa mbogamboga.

Aidha, Denis Innocent, Katibu wa Kata ya Gumbiro, ambaye alizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kijiji cha Ngadinda, aliipongeza serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kupeleka mradi huo mkubwa katika eneo hilo. Alisema kuwa mradi huu utasaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji hicho.

Mradi huo wa maji ni moja ya hatua muhimu za kuhakikisha wananchi wa Madaba wanapata huduma muhimu za kimaendeleo, na umekuja kama suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji katika kijiji hicho.

Related Posts