Huwezi kuamini lakini ndivyo ilivyo kwamba Rais wa Marekani Donald Trump amesema Ukraine isahau kujiunga na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), tamko ambalo ni pigo kwa Ukraine ambayo katika azma hiyo awali iliungwa mkono na Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden.
Katika mkutano na waandishi wa habari juzi, Trump alipuuzilia mbali uwezekano wa Ukraine kujiunga na NATO na akamuambia Zelensky kwa anaweza kusahau kuhusu hilo.’
“Pengine ilikuwa ni sababu ya jambo hili zima kuanza,” amesema, akikiri kuwa kujitanua NATO upande wa mashariki ni moja ya sababu za kuanza kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.
Haya yanajiri huku televisheni ya CNN ya Marekani ikitangaza kuwa Marekani imejitenga na nchi za Magharibi kuhusu suala la Ukraine, na hili ndilo jambo lililobadilishwa na Rais Donald Trump kuhusu nafasi ya Marekani kimataifa. Ripoti ya CNN imeongeza kuwa, mwelekeo wa kutatanisha wa Trump kwa Rais Putin wa Urusi na kujitenga na Ukraine umevuruga miungano ya zamani na kuanzisha ushindani wa washirika na wapinzani wa Marekani kwa ajili ya kuunda makubaliano ya amani ambayo anakusudia kufanya na Rais wa Urusi.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, serikali ya Marekani imeitaka Ukraine kukabidhi haki za uchimbaji wa madini adimu ya nchi hiyo kama fidia ya msaada uliotolewa kwa nchi hiyo katika kipindi cha miaka kumi na moja iliyopita. Trump anasema Ukraine inadaiwa na Marekani kiasi cha dola bilioni 500.