Bilionea Elon Musk ametangaza hadharani kuunga mkono wazo la Marekani kujiondoa Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO).
Akijibu ujumbe wa mtandao wa kijamii unaotetea hatua hiyo janaJumapili, Musk, ambaye anaongoza Idara ya Ufanisi wa Serikali ya Marekani (DOGE), amesema, “Ninaafiki.”
Rais wa Marekani, Donald Trump na wabunge wa chama cha Republican wameapa kutazama upya uanachama wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, na pia katika jumuiya ya kijeshi ya NATO, inayoongozwa na Marekani. Mnamo Februari, Seneta Mike Lee wa Utah aliwasilisha mswada wa Sheria ya Kujitenga Kabisa na Mtanziko wa Umoja wa Mataifa), akipendekeza kujiondoa kikamilifu kwa Marekani Umoja wa Mataifa.
Lee aliukosoa Umoja wa Mataifa na kulitaja kama jukwaa la madhalimu ambalo linaihujumu Marekani na washirika wake, akisema kuwa licha ya ufadhili mkubwa kutoka Marekani, lakini shirika hilo limeshindwa kuzuia vita, mauaji ya halaiki, ukiukaji wa haki za binadamu na majanga.
Akirejelea matamshi hayo ya Seneta Lee, Musk ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, “Marekani hutoa ufadhili mkubwa kwa UN na taasisi zinazofungamana nayo.”
Msimamo wa bilionea huyo unalandana na wa Trump, ambaye mara kwa mara amekuwa akiikosoa NATO, akiwataka wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza bajeti za ulinzi, na kutishia kujiondoa, akisema Marekani inabeba mzigo usio wa haki wa kifedha kwa usalama wa Ulaya.