Jeshi la Uganda limethibitisha kutuma kikosi chake katika mji wa Mahagi, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ili kukabiliana na makundi ya waasi kwenye eneo hilo. Hatua hii inakuja wakati kukiwa na wasiwasi kwamba vita vya Mashariki mwa Kongo vinaweza kuenea na kuwa mgogoro wa kikanda.
Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulayigye, amesema kikosi hicho kimeingia Mahagi baada ya ombi kutoka kwa jeshi la Kongo, kufuatia madai ya mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa na waasi wa kundi la CODECO. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu operesheni hiyo.
Mahagi, uliopo katika mkoa wa Ituri mpakani na Uganda, umeshuhudia mashambulizi makubwa, ambapo watu 51 waliuawa Februari 10 na wapiganaji wa CODECO, kwa mujibu wa vyanzo vya mashirika ya kibinadamu na wakazi wa eneo hilo.