Rais Donald Trump wa Marekani, ametishia kusitisha ufadhili wa serikali ya shirikisho kwa vyuo vikuu au taasisi zozote za elimu zinazoruhusu maandamano kufanyika kuwaunga mkono Wapalestina.
Trump alitoa onyo hilo kupitia jukwaa lake la mitandao ya kijamii, Truth Social juzi Jumanne, baada ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina kujitokeza nje ya Chuo Kikuu cha Columbia, New York, nchini Marekani.
Mtawala huyo wa Marekani ameandika: “Ufadhili wote wa serikali ya shirikisho utasitishwa kwa vyuo, shule au taasisi yoyote ya elimu inayoruhusu maandamano haramu.”
Aliendelea kusema kuwa “wachochezi” watatiwa gerezani au kufukuzwa kabisa kurejea katika nchi walikotoka. Aliongeza kuwa wanafunzi wa Kimarekani watatimuliwa kabisa chuoni au, kulingana na uhalifu wao, watakamatwa.”
Ingawa hakutaja moja kwa moja maandamano ya wanaounga mkono Palestina, Trump hapo awali alikuwa ametishia kuwafukuza Marekani wanafunzi wowote wanaoshiriki maandamano dhidi ya Israel na wanaopinga mauaji ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.