Dar es Salaam. Kauli yenye tuhuma iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla imezusha sintofahamu huku wadau wakiwamo viongozi wa kisiasa wakimtaka ajitokeze kutoa ushahidi au aombe radhi.
Juzi, Makalla akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Simiyu, alitoa shutuma dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa wamepanga kutumia fedha wanazochangisha kupitia kampeni yake ya Tone Tone, kununua virusi vya Ebola na Mpox kisha kuvisambaza nchini.
“Hawa watu hasa viongozi waandamizi ambao familia zao hazipo Tanzania wanataka kutumia michango ya Tone Tone eti kufika wakati, wakanunue virusi vya Ebola na Mpox ili visambae Tanzania na uchaguzi usifanyike,” amedai Makalla.
Makalla ambaye amewahi kuwa naibu waziri wa wizara mbalimbali na mkuu wa mkoa, amesema, “hili ni jambo la hatari, Chadema na wenyewe wapo watakaokufa kwa jambo hili, lakini wenzetu wengine hawana familia hapa Tanzania tushindane kwa hoja.”
Kutokana na kauli hizo, Mwananchi imemtafuta Makalla jana Jumapili Machi 23, 2025 lakini jitihada hazikuzaa matunda.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wamehoji kauli hizo huku wakimtaka kuthibitisha au kuomba radhi kwa kuzusha taharuki.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo za Makalla, amesema hawezi kumjibu kwa kuwa kufanya hivyo ni kumpa heshima asiyostahili.
“Kaka huo ujinga wa Amos Makalla nitaujibuje mimi, kumjibu ni kumpa heshima asiyostahili,” amesema Lissu.
Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda amesema kauli hiyo ni hatari kwa siasa za Tanzania inayojiandaa kufanya uchaguzi wake baadaye mwaka huu.
“Hizo ni tuhuma nzito kutolewa na kama hilo ni kweli, viongozi wa Chadema wangepaswa kukamatwa na chama kufutiwa usajili, lakini hata Makalla mwenyewe anaonekana haiamini kauli yake,” amesema Dk Nyamsenda.
Kwa uzito wa tuhuma hizo, Dk Nyamsenda amesema Makalla anapaswa atafutwe kuthibitisha kauli yake na kama hana uthibitisho anastahili hatua sio tu ndani ya chama chake, bali hata za kisheria.
Pia, ameichukulia kauli ya Makalla kama mbinu za CCM kuwakatisha tamaa Watanzania wanaoiunga mkono Chadema.
Kiongozi mstaafu wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kauli ya Makalla haina afya kwenye siasa za Tanzania na anapaswa kuomba radhi kwa umma.
Zitto amesema kauli hiyo ni hatari hasa wakati huu nchi ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu.
“Hii kauli ni ya hatari sana, sio kauli ya kiuenezi bali ni ya kinazi na anapaswa kuomba radhi haraka,” amesema Zitto.