Walimu Mbeya kupelekwa Dubai ‘kutalii’

Mbeya. Serikali mkoani Mbeya imefanya jambo la kipekee kwa walimu waliosaidia kuboresha kiwango cha ufaulu wa masomo katika shule za msingi na sekondari kwa kuwapeleka Dubai.

Walimu hawa watajifunza na pia kupata fursa ya kutalii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuboresha elimu katika mkoa huo.

Ahadi hiyo ilitolewa Julai 16 mwaka jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, wakati wa kikao cha tathmini ya elimu kilichohusisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk Homera alieleza kuwa Serikali Mkoa wa Mbeya itawapeleka walimu 10 bora watakaofanikisha kuboreshwa kwa ufaulu wa masomo.

Kwa mujibu wa Dk Homera ahadi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha kiwango cha elimu na kuthamini mchango wa walimu katika kuendeleza sekta ya elimu mkoani humo.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo Machi 24 wakati wa futali iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Homera amesema hadi sasa walimu 10 tayari wapo Dubai kwa ajili ya kujifunza na kutalii.

Amesema kuwa walimu hao ni wale walioonyesha mafanikio katika kuboresha ufaulu wa masomo katika shule za msingi na sekondari za Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Wilaya ya Rungwe na wako huko wakiongozwa na Ofisa Elimu Mkoa huo.

“Matokeo ya darasa la saba tulishika nafasi ya pili, kidato cha nne tukawa wa kwanza, mwakani zawadi zitaendelea, hadi sasa walimu 10 wa msingi watano na sekondari watano wapo Dubai.

“Hii imetokea Mbeya pekee nchini, mwakani zawadi zitaendelea kutengeneza motisha zaidi hii ni kwa niaba ya wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya katika kuongeza ufaulu kwa shule zetu,” amesema Dk Homera.

Mkuu huyo amewatoa hofu wananchi kuwa miundombinu inayoendelea kujengwa, ikiwamo ya barabara ya njia nne na mradi wa maji Mto Kiwira na miradi mingine itakamilika ndani ya kipindi cha awamu ya sita.

“Kwa maana hiyo msisikilize sana maneno ya watu huko pambeni kwamba barabara imekwama, niwahakikishie hii miradi itakamilika ndani ya kipindi hiki cha awamu ya sita,” amesema Dk Homera.

Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ayas Njalambaha amesema kwa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, wananchi wanapaswa kuliombea Taifa kuhakikisha mchakato huo unaanza na kuisha salama.

“Sisi viongozi wa dini tutazidi kuliombea Taifa haswa kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, wananchi tuungane katika hili kila mmoja kwa imani kuhakikisha tunafanikisha kwa pamoja,” amesema Njalambaha.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani mkoani Mbeya, Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Mwakwama amesema wamekuwa na ushirikiano mkubwa na Serikali ya Mkoa huo haswa kwenye suala la maendeleo.

“Linapokuja suala la maendeleo tunaweka upinzani pembeni kwa kuwa wote tunawatumikia wananchi, tukupongeze Mkuu wa Mkoa na tukuombee safari njema katika harakati zako, ushirikiano huu uwe endelevu,” amesema Mwakwama.

Related Posts