John Mrema Alaani Shambulio la Mwenezi Bawacha – Global Publishers

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, ameonesha masikitiko yake kuhusu taarifa iliyotolewa na chama hicho kuhusiana na tukio la shambulio dhidi ya kiongozi wa wanawake taifa wa chama hicho (BAWACHA). Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), Mrema alieleza sababu kadhaa zilizomfanya kutoridhishwa na taarifa ya chama.

Mrema ameeleza kuwa chama hakikuona haja ya kulaani kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na kuumizwa na mwanaume, badala yake kinadai kuwa ni taarifa zinazosambazwa mitandaoni. Alisema kuwa hatua hii inaonesha kutokuwepo kwa mshikamano wa ndani ya chama na kutojali hali ya mwanachama aliyeathirika.

Aidha, ameeleza kushangazwa na chama kushindwa kutoa pole kwa kiongozi huyo, ikizingatiwa kuwa mara kadhaa kimekuwa kikitoa pole hata kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapopatwa na majanga.

Sambamba na hilo, amesema kuwa kutotoa pole kwa mgonjwa kunaleta maswali kuhusu utamaduni wa chama katika kushughulikia masuala ya ndani.

Mrema pia amelalamikia kauli ya chama inayodai kuwa kinachunguza tukio hilo, huku wakati huo huo kikitoa vitisho kwa mhanga wa shambulio hilo. Alieleza kuwa hatua hiyo inazua taharuki na inaweza kuathiri upatikanaji wa ukweli kuhusu tukio husika.

Zaidi ya hayo, Mrema amekosoa kauli za chama ambazo alizilinganisha na kauli zilizokuwa zikitolewa wakati wa uongozi wa Hayati John Magufuli, akihusisha na matukio ya watu kupotea na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Katika tamko lake, Mrema amesisitiza kuwa analaani vikali kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na wanaume, akikitaja kuwa ni ukatili wa kijinsia unaopaswa kupingwa na kila mtu mstaarabu bila kujali ni nani aliyekumbwa na tukio hilo.

Ameongeza kwa kusema kuwa ukatili huu hauna tofauti na vitendo vingine vya kikatili vinavyowakumba wanawake nchini, na hivyo akatoa wito wa mshikamano wa pamoja katika kupinga matendo kama haya, ndani na nje ya vyama vya siasa.

Related Posts