Wafanyabiashara kunufaika mikopo nafuu | Mwananchi

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo watakuwa na uhakika wa kupata mikopo nafuu isiyo na dhamana baada ya taasisi za kifedha EFTA na GSM kuingia mkataba wa kifedha kuwezesha suala hilo.

Sasa wafanyabiashara watakuwa na uwezo wa kupata mikopo ya vifaa, magari na vitendea kazi ili kujiimarisha kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 8, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za GSM, Benson Mahenya alipozungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano na EFTA.

Amesema wameamua kushirikia kulitekeleza hilo, baada ya kutambua umuhimu wa shughuli za uzalishaji wanazozifanya pamoja na wateja wao.

Mahenya amesema kupitia mkataba huo, mawakala na wadau wanaosambaza bidhaa zao, lakini wanakosa mikopo kwa vigezo vya kawaida, watakopeshwa magari kutoka EFTA kupitia dhamana zao.

“Naamini kwa kufanya hivi tutagusa maisha ya kila mtu na kuongeza thamani ya biashara kwa wadau wetu na kuongeza msaada,” amesema.

Kutokana na shughuli nyingi wanazofanya ikiwamo uzalishaji wa vinywaji, amesema wafanyabiashara hao wataokopeshwa, watasaidia katika kuimarisha usafirishaji wa matunda kama malighafi ili kuondoa uharibifu.

“Sisi tumeona ni vyema tukaimarisha usafirishaji wa matunda kwa kwenda eneo la uzalishaji ili yasiharibike na kupotea pia kumpa thamani mkulima,” amesema.

Mkuu wa Mauzo na Masoko wa EFTA Tanzania, Clerius Asiel amesema kwa zaidi ya miaka 20 wamekuwa nguzo muhimu kwa wafanyabiasha wadogo na kati nchini, wakiwasaidia kumiliki mashine na magari kwa mikopo nafuu bila dhamana.

Ameeleza mkataba huo na GSM umekuja baada ya kuwezesha upatikanaji wa magari  60 ya kusambaza bidhaa za kampuni hiyo.

“Hatua hii ni kielelezo cha maono yetu ya pamoja ya kukuza biashara endelevu, huku tukiwa na mchango wa moja kwa moja katika uundaji wa ajira na kuboresha kipato kwa wafanyabiashara wadogo,” amesema.

Kwa makubaliano hayo, amesema watapata nafasi ya kufanya biashara na wadau wote.

Amesema mwaka jana pekee wametumia Sh48 bilioni kwa wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali.