Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu Dkt. Dorothy Gwajima.
…………….
Na Daniel Limbe,Chato
“Kuna watu aina mbili ambao watakwambia huwezi kuleta mabadiliko ulimwenguni, ambaye anaogopa kujaribu kufanya jambo na yule anaehofia utampiku kwenye jambo hilo,”
Ni kauli ya Mwanafalsafa wa Marekani Ray Goforce ambaye alikuwa akisisitiza jamii kufanya tafakuri njema katika harakati za kuyasaka mafanikio na kupuuza kauli zenye kukatisha tamaa.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine, umaskini na hali duni ya kiuchumi vinaathiri sana usawa wa kijinsia.
Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ndizo zenye maskini wengi zaidi duniani,huku wengi wao wakiwa wanawake.
Kwa hali hiyo tunahitaji mipango madhubuti ya kuwawezesha wanawake ki uchumi na kuwaongezea kipato.
Hatuwezi kukataa kwamba wanawake wamebeba na wanaendelea kubeba mizigo mikubwa ya kazi shambani na nyumbani kutokana tu jinsia yao.
Wamenyimwa haki yao ya usawa kwa sababu ambazo hazihusiani hata kidogo na mchango wao kwa ustawi wa familia,nchi na dunia kwa ujumla.
Licha ya mipango mizuri inayo tekelezwa na serikali pamoja na wadau wengine wa Maendeleo, wapo baadhi ya watu ambao kazi yao kubwa ni kukatisha tamaa na wengine wakitamani mipango hiyo ya serikali kuwawezesha wanawake ki uchumi isifanikiwe.
Mbali kuwatia unyonge,hali hiyo inadhoofisha maendeleo ya familia kutokana na ukweli kwamba mwanamke anapojikomboa kifikra,ki elimu, kiuchumi na kiutamaduni ni sawa na kulikomboa taifa.
UTAFITI KATIKA KIPATO
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kuhusiana na watu wenye uwezo wa kufanya kazi Tanzania(ILFS) kwa mwaka 2021,mbali na mambo mengine ulibaini kuwa wanaume wana kipato kikubwa kwa mwezi kuliko wanawake.
Ilionyesha kuwa wanaume wanapata wastani wa shilingi 396, 885 kuliko wanawake ambao wanapata kwa wastani wa shilingi 378, 469 katika aina zote za ajira ikihusisha kazi zenye ujira au ajira binafsi katika sekta ya kilimo.
Kwa utafiti huo ni wazi kuwa wanawake wengi waliopo kwenye ajira walikuwa wakilipwa ujira wa chini, huku wengine wakijishughulisha na ajira nyingi zisizo rasmi na zenye ujira mdogo ikilinganishwa na wanaume.
Kutokana na hali hiyo,serikali ikasisitiza kila halmashauri ya wilaya,Manispaa na Miji nchini, kutekeleza mpango wa kutenga fedha aslimia 10 kutoka mapato ya ndani ili kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake aslimia (4) vijana aslimia (4) pamoja na na watu wenye ulemavu aslimia (2).
Katika utekelezaji wa agizo hilo,halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita ikalazimika kusimamia kikamilifu takwa la serikali ili kuhakikisha wananchi hao wanajikwamua na lindi la umaskini wa vipato.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kuhusiana na mikopo iliyolenga kuinua uchumi wa wanawake kwa mwaka 2021/22 jumla ya vikundi 34 vilipewa mikopo ya kiasi cha shilingi milioni 180,000,000 kati ya milioni 311,000,000 zilizotengwa kwaajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Kadhalika katika bajeti ya mwaka 2022/23 jumla ya vikundi 20 vya wanawake vilinufaika na kiasi cha shilingi milioni 132,000,000 kati ya milioni 285,000,000 zilizotolewa kwa wanufaika wa mikopo hiyo.
Aidha jumla ya vikundi 31 vya wanawake vilinufaika na kiasi cha shilingi milioni 190,000,000 kati ya shilingi milioni 475,000,000 zilizotolewa na halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa lengo la kukuza uchumi na kuimalisha usawa wa Kijinsia katika jamii .
MAONI YA WANANCHI
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa Makala hii wamekuwa na mitazamo mbalimbali huku baadhi yao wakitaka serikali kuwapatia wanawake mitaji itakayoweza kuwakomboa ki uchumi.
Semen Stephano,mkazi wa mjini Chato,anasema vuguvugu la usawa wa kijinsia limekuwa likizungumzwa sana lakini ugumu wake unatokana na historia iliyolenga kumnyanyasa mwanamke.
“Tawala tofauti zimekuwa na namna ya kulishughulikia suala la haki za wanawake, lakini mara zote ni kundi ambalo limekuwa likipata shida na taabu kwa kile kinachoitwa viumbe dhaifu,”
“Ukweli ni kwamba tabaka hili la wanawake limebeba maisha ya watu wengi sana hapa duniani,wenye elimu na wasio nayo lakini ndiyo kundi pekee linaloonekana muhimu wakati wa kuleta watoto duniani na baada ya hapo thamani yake hupotea” anasema Semen.
Neema Nestory,anasema maisha ya wanawake yamekuwa ya wasiwasi kwa miaka mingi,licha uwepo wa Sheria mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kiuchumi,kwa madai utekelezaji wake ni mdogo hasa katika maeneo ya vijijini.
Anasema ujasiri kamili wa mwanadamu ni Uchumi na elimu na kwamba kutokana na ukosefu wa mambo hayo mawili ndiyo kisababishi kikuu cha wanawake kunyanyasika na kukosa usawa wa kijinsia.
“Bila kudandanyana heshima ya mtu ni pesa,ikichagizwa na elimu inamfanya ajiamini, kujipenda na kujithamini utu wake,”
“Mie nachoweza kusema katika suala zima la usawa wa kijinsia ni kumwezesha mwanamke ki uchumi kwa kumpatia mikopo yenye masharti nafuu sambamba na kumpatia elimu ya biashara,maana wanawake wengi tunafanya biashara ndogo (machinga) na zenye faida kidogo” anasema Neema.
Kadhalika Merissa Erasto, anasema licha ya kundi la wanawake kuwa ndiyo kubwa katika ajira zisizokuwa rasmi katika jamii,bado wanakabiliwa na changamoto nyingi za kuwakatisha tamaa ikiwemo kuhamishwa ovyo katika maeneo mbali mbali ya biashara zao.
“Matukio haya si mageni machoni mwetu,hasa kwa sisi machinga ambao bado tunajitafuta kwa mitaji midogo,mambo haya yamekuwa yakijirudia rudia,ikitokea utulivu ni kwa muda mchache kwa kisingizio kuwa tunachafua Mazingira,”
“Hatua hii inatukatisha sana tamaa,lakini tukitazama nyuma kuona kundi linalo tutegemea tunalazimika kuendelea kupambana katika mazingira magumu, na baadhi yetu tunaishi kwa mikopo yenye riba kubwa kutoka taasisi binafsi za kifedha.”
Anapendekeza serikali kuja na mpango kabambe wa kuwatembelea wanawake na kuwapa elimu ya kibiashara kabla ya kuwapatia ruzuku au mikopo isiyo kuwa na riba jambo litakalo rejesha utulivu kwa wanawake kuelekea usawa wa kijinsia.
“Tutumie muda wetu vizuri kutafakari namna bora ya kuwainua wanawake katika usawa wa kijinsia,mikopo mingi inayotolewa inawanufaisha wanawake wachache hasa walioko mijini ukilinganisha na vijijini”anasema Suleiman Hassan.
Ukweli hatuwezi kukataa kuwa wanawake wamebeba maisha ya familia nyingi hapa Tanzania huku wakiendesha shughuli zao kwa mitaji midogo na walio wengi haizidi sh 500,000 kushuka chini hadi sh 100,000.
Kutokana na hali hiyo kama taifa hatuna budi kuondokana na mtazamo wa kuwa mwanamke hawezi kulinganishwa na mwanaume badala yake wasaidiwe kupata mitaji ili wainue uchumi wao na kuwaondoa kwenye fedheha ya mikopo umiza inayo dharirisha utu wao.
“Hapa ni muhimu kwa watu waliopewa dhamana na wananchi,lazima wapiganie haki za wanawake katika mikopo ili waanzishe biashara na wenye nazo wakuze mitaji yao badala ya kubaki na maneno yasiyokuwa na utekelezaji” anasema Hassan.
Stephano Katemi,anaitaka jamii kubadili mtazamo hasi kwa wanawake badala yake watoe nafasi ya kuwasikiliza na kuwapa fursa muhimu za kujiendeleza ki elimu na ki uchumi.
Anasema ni muhimu tuwatambue kuwa wanaweza na tushauriane nao kulingana na aina za biashara zao na wapi wanaona inaweza kuwa sehemu muhimu kwao kibiashara badala ya kuwafukuza pasipo kutazama kundi linalowategemea.
KAULI YA WAZIRI GWAJIMA
Aprili 8,2025 Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wanawake na Makundi maalumu,Dkt. Dorothy Gwajima akawataka wanawake kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji ki uchumi ili kuwasaidia kuzifahamu fursa zilizopo nchini.
Ni baada ya kupokea Makala 1000 za mwongozo wa uundaji na uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka Benki ya Biashara Tanzania(TCB).
Dkt. Gwajima, anasema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuona wananchi wanazifahamu fursa zilizopo za kujikwamua kiuchumi ikiwemo kundi la wanawake.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikitekeleza jukumu la kuwawezesha wanawake ki uchumi, kutokana na uzoefu wa utekelezaji huo ilifanya mapitio ya mwongozo wa majukwaa ya Uwezeshaji wanawake kiuchumi wa mwaka 2022 na toleo la mwaka 2024 linaloendana na mahitaji ya sasa”anasema.
Aidha Dkt. Gwajima nasema Tanzania imeweka misingi kwenye Katiba ya nchi kuhusu ajenda ya maendeleo yenye usawa wa kijinsia na mahsusi uwezeshaji wanawake na wasichana kupitia sekta mbalimbali.
Kadhalika uwepo wa Sheria ya Manunuzi ya Umma inayohakikisha aslimia 30 ya zabuni zinawanufaisha wanawake na Makundi maalumu.
Pia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotaka mamlaka hizo kutenga aslimia 10 ya mapato ya ndani kwaajili ya mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu pamoja na Sera ya Taifa ya Biashara inayohakikisha usawa wa kijinsia kwenye Biashara, zimekuwa chachu ya kuinua uchumi kwa wanawake.
Aidha katika tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani,zinaonyesha kuwa usawa wa kijinsia ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.
Kutokana na ukweli huo,mwaka 2024 Benki ya Dunia iliipatia serikali ya Tanzania mkopo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 sawa na takribani shilingi bilioni 248,kwaajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa kukuza usawa wa kijinsia nchini.
Miongoni mwa fedha hizo kiasi cha dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada, na kiasi cha dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu utakao wanufaisha wanawake takribani 319,850.
NINI KIFANYIKE
Baadhi ya wadau wa maendeleo, Winfrida Rwegoshora, anasema serikali iboreshe mfumo wa utoaji mikopo kwa wanawake hasa walioko vijijini.
“Umaskini wa vipato kwa wanawake unaweza kutokomezwa na kuinua usawa wa kijinsia iwapo watawezeshwa mikopo isiyokuwa na riba”anasema Winfrida,” na kuongeza kuwa.
“Elimu ya kifedha itolewe kwa wanawake kabla na baada ya kuwapatia mikopo isiyo kuwa na riba.”
Shani Athumani anashauri serikali iwatengenezee mazingira mazuri ya kufanya biashara badala ya kuwahamisha kila wakati kwa madai ya kuchafua miji.
Anahitimisha kwa kuitaka jamii kuwaamini na kuwathamini wanawake katika harakati za kutafuta usawa wa kijinsia.
Mwisho.