Wataalamu kujadili teknolojia matibabu vidonda vya tumbo

Dar es Salaam. Ikiwa ni hatua ya kuelekea kuboresha matibabu ya vidonda vya tumbo, wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa chakula wanatarajia kukutana kwenye kongamano la kisayansi litakalofanyika Mei 24, 2025, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa matibabu ya vidonda vya tumbo yanahusisha vipimo vya haja kubwa na damu kwa sehemu kubwa, ingawa zipo njia mpya ikiwemo kifaa cha kupuliza (Urea Breath Test) na matumizi ya kamera zilizoingizwa tumboni.

Wataalamu hao kutoka Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki watajadiliana namna ya kutumia bunifu hizo za kisayansi ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Hatua hiyo imetajwa kupambana na maradhi ya mfumo wa chakula kama anavyosema Dk Muhidin Mahende, Katibu Mkuu Taasisi ya JamiiBora Health Service Network.

Akizungumza jana Aprili 15, 2025 jijini hapa, Dk Mahende amesema dunia kwa sasa ipo katika matumizi ya sayansi na teknolojia za hali ya juu katika matibabu, hivyo ni wakati wa kwenda nayo sambamba.

“Sasa hivi tunapima vidonda kupitia choo kikubwa na damu lakini kuna teknolojia mpya iliyokuja ya kipimo cha kupuliza ingawa haijaenea kama inavyohitajika.

“Kipimo cha kupuliza (Urea Breath Test) kinachotoa majibu kama muhusika ana wadudu au hana kupitia kupumuliwa ambayo imeingia hivi sasa ndiyo tunapaswa kwenda huko,” amesema.

Akitaja njia nyingine za utambuzi wa ugonjwa huo  amesema kuna matumizi ya kamera yenye taa (OGD), kwa ajili ya kumulika kuangalia hatua vilivyofikia kama vimekaribia kutoboa mfuko wa chakula.

Matumizi ya njia hizo na nyingine watakazojadili ndizo zilizopo duniani kwa sasa. Amesema zinahitajika kuingia kwa wingi nchini ili kupambana na maradhi hayo.

Aidha, amesema matumizi ya njia hizo za kisasa zitasaidia kugundua mapema dalili ambapo mgonjwa akigundulika na kutumia dawa mapema ugonjwa hautafikia hatua mbaya.

Akielezea sababu na athari za vidonda vya tumbo Dk Mahende amesema kwanza unasababishwa na bakteria aitwaye (Helicobacter pylori (H. pylori) wanaokaa kwenye maji ama vyakula visivyo salama.

“Bakteria hawa akiingia anaathiri ukuta wa mfuko wa tumbo uliotengenezwa na utandu unaokinga asidi inayotumika kumeng’enyea chakula.

“Bakteria akija anaathiri huu utandu anauharibu halafu asidi hiyo inaanza kuathiri mfuko wa tumbo unatengeneza vidonda,” amesema.

Mtaalamu huyo amesema kuna uwezekano wa hayo kutokea ukiwa na miaka 12 halafu madhara yakaanza kujitokeza ukiwa na miaka 20. Kwa maana kuchukua muda mrefu.

“Dalili zake mwanzo utasikia tumbo linauma, kichefuchefu, homa lakini changamoto inakuja pale utakapopuuzia dalili hizo. Ukiwahi hizo dalili ungeweza kupima na kunywa dawa kabla ya athari zaidi,” amebainisha.

Dk Mahende amesema changamoto ya watu wengi wakihisi dalili wanatumia dawa kutuliza maumivu kisha wanapuuzia huku wakiwa hawajui ni hatari kwao.

“Tutajadili kwa kina namna tunavyoendeleza sayansi, ubunifu katika eneo la magonjwa ya mfumo wa chakula changamoto na tunavyoweza kupambana nayo,” amesema.

Aidha, amesema wagonjwa wa vidonda wanaumwa tumbo mara nyingi, tumbo kujaa gesi, kutostahimili kukaa na njaa, kushindwa kula baadhi ya vyakula.

“Athari za vidonda moja wapo ni kutoboka kwa mfuko wa chakula/utumbo pia saratani inayotokana na kuugua kwa muda mrefu. Mfano mtu anaumwa tangu akiwa na miaka 20 akifika miaka 55 matokeo yake vidonda vinavyouma na kujirudiarudia kwa kuchubua hatimaye wakati mwingine vinasababisha saratani,” amesema.

Akitaja uwezekano wa kurithi, Dk Mahende amesema kwa upande wa watoto wanaweza wakaugua endapo mama na baba wana ugonjwa huo.

“Mtoto atapata ugonjwa huu kwa asilimia 50 kama wazazi wake wanao na endapo akipata bakteria hao wasababishi,” amesema.

Kutokana na hayo amesema watajadili kuja kwa mbinu mpya za kisayansi kusaidia kupunguza ugonjwa huu pamoja na uelekeo wa baadaye wa kupambana na maradhi ya mfumo wa chakula.

Mratibu wa kongamano hilo, Ally Nchahaga amesema watu wanapaswa kujumuika pamoja siku hiyo kwa ajili ya kuisaidia jamii mbinu mpya zitakazotumika hadi vijijini.

Amesema wanahitajika wataalamu wa mfumo wa chakula (Gastroenterology), wataalamu tiba na afya shirikishi, wanafunzi wa afya, wamiliki wa hospitali wasambazaji wa dawa waratibu wa huduma za afya, wananchi na taasisi za Serikali. Kushiriki kongamano hilo.